• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 2:53 PM
VIWANDA NAKURU: Kampuni zilivyofungwa kwa kulemewa na madeni

VIWANDA NAKURU: Kampuni zilivyofungwa kwa kulemewa na madeni

NA RICHARD MAOSI
MJI wa Nakuru unapojizatiti kupata hadhi ya kuwa jiji, vijana wengi bado hawana jambo la kujivunia kwa sababu ya nafasi haba za ajira.
 
Mji wa Nakuru ni wa nne kwa ukubwa nchini baada ya Nairobi, Kisumu na Mombasa. Vilevile ni makao makuu ya jamii za bonde la ufa.
 
Uwekezaji katika sekta ya viwanda aidha umepungua, kutokana na madeni kutokana na mikopo ya benki, huku wafanyakazi waliopigwa kalamu bila mshahara wakielekea kortini kusaka haki ya malipo yao.
 
Viwanda vingi vimegeuzwa kuwa sehemu za kufanyia biashara ndogo ndogo,  huku majengo ya mashirika ya kibinafsi yakiuzwa.
 
Taifa Leo Dijitali iligundua viwanda vingi vimegeuzwa sehemu za kuhifadhi bidhaa kwa bei nafuu.
 
Muungano wa Watengenezaji wa Bidhaa (KAM) uliweka matawi yake mengi kaunti ya Nakuru 1966, miaka michache tu baada ya Kenya kupata uhuru lakini sasa taswira ni tofauti.
Wafanyikazi nje ya Shirika la Reli katika Kaunti ya Nakuru wakisemezana. Mnamo mwaka wa 2006 idadi yao ilikuwa 2000 lakini sasa ni 20. Picha/ Richard Maosi
 KAM ilipaswa kuwaleta pamoja wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuwarahisishia uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zao kwa masoko ya humu nchini na nje.
 
Hata hivyo, ilileta mshikamano baina ya wakulima na wateja, katika hatua ya kuinua uchumi wa taifa.
 
KAM iliungana na Muungano wa Wakulima nchini (KFA) ili kuwatafutia wakulima soko la mazao yao lakini sasa ofisi zake zimefungwa na mali yake kupigwa mnada.
 
Pia ofisi za Bodi ya Pareto nchini (PBK) zilikuwa zimechina lakini sasa zimeanza kurudia huduma za awali serikali ya kaunti ilipoamua kukifufua kilimo cha pareto ili wakulima kutoka Molo wapate sehemu ya kuuza mazao.
Wapita njia wameanza kuiba vyuma kwenye baadhi ya maeneo ya viwanda yaliyobakia kuwa mahame. Picha/ Richard Maosi
 Kampuni za kuzalisha pareto wakati mmoja zilikuwa zikiongoza kote nchini kwa uzalishaji lakini zikalemewa na madeni mengi ndipo zikafungwa.
Taifa Leo Dijitali ilizungumza na Amos Nyakundi ambaye alikuwa mfanyikazi kwenye kampuni ya kukuza pareto.
 
Anasema aliwaona watu wengi wakipoteza ajira na wengine kujifia majumbani mwao kutokana na hali ngumu ya maisha na ukosefu wa malipo ya uzeeni.
 
“Familia nyingi zimetaabika kuanzia mwanzo wa miaka ya tisini hadi 2000, na viongozi wao wamekuwa wakitumia nafasi hizo kujipigia siasa lakini waingiapo mamlakani waliwasahau raia,” akasema.
Familia nyingi zilizotegemea kampuni za mji huu kwa riziki zimesalia bila ajira baada ya mazingira ya biashara kuharibika.  Picha/ Richard Maosi
 Kwa upande mwingine, kampuni ya magari iliyofahamika kam Sam-con-Assembly, Flamingo Bottlers na kampuni ya nyanya iliyokuwa katika eneo la Kabazi, ni baadhi ya kampuni tajika zilizolemewa na madeni na kufunga biashara.
 
Millicent Cherotich, mfanyikazi wa Shirika la Reli anakumbuka vyema miaka ya nyuma ambapo shughuli za kibiashara zilikuwa zimenoga katika kaunti ya Nakuru kutokana na usimamizi bora.
 
Enzi hizo mtu aliheshimika sana endapo angetambulika kuwa alikuwa akifanya kazi katika shirika la reli nchini.
 
Anakumbuka kwa majuto masaibu ya kampuni ya betri, Eveready, ambayo ilifungwa baada ya China kuanza kuleta betri za bei nafuu na za huku nchini zikaanza kukosa soko.
Hili ndilo bohari lililokuwa likitumika kuhifadhi maharagwe lakini limebakia kuwa msitu wa mimea baada ya shughuli kusitishwa. Picha/ Richard Maosi
 Aidha kampuni ya kutengeneza magari ya Sam Con Limited iliyohusika katika uundaji wa malori ilihamia mjini Nairobi na kubakisha majengo tu.
 
“Fahari ya mji wa Nakuru imepotea kilichobakia ni dhidi ya vijana wengi wanaotaabika wakisaka ajira ili waweze kuziendeleza familia zao,” alisema.
Aidha kampuni ya Kabazi iliyokuwa ikitumia nyanya kutengeneza Tomato paste ilifunga na kuwaacha wakulima wakihangaika..
 
Wakulima wengi walipoteza ajira na kugeukia aina nyingine ya ukulima na kurudisha nyuma uchumi wa eneo la Subukia viungani mwa mji wa Nakuru.
Zilizokuwa ofisi za kampuni ya Unga Limited sasa ni stoo ya kuhifadhi mahindi. Picha/ Richard Maosi
 Aidha anakumbuka fika kampuni ya kutengeneza mikate ya Elliots Bakeries ambapo zaidi ya wafanyikazi 600 waliachishwa kazi,ghafla bila notisi.
 
Usimamizi wa kampuni ulisema walifikia uamuzi huo ili kupunguza kiwango cha hasara kilichokuwa kikiendelea kushuhudiwa.
 
Kufikia 2015 watu zaidi ya milioni moja kutoka kaunti ya Nakuru hawakuwa na ajira wengi wao wakiwa ni vijana na wale wenye familia changa.
 
Inaaminika kuwa katika sekta ya kilimo kaunti ya Nakuru inapatikana katikati ya taifa na ni muhimu kwa kutoa bidhaa zinazotegemewa katika maeneo mengine.
Kampuni ya Eveready iliyofungwa baada ya Uchina kuwaletea ushindani mkali walipoanza kutoa kawi ya bei nafuu. Picha/ Richard Maosi
 Baadhi ya viwanda katika kaunti ya Nakuru bado vinaendelea kudumu huku vingine vikininginia ama kubakia tupu shughuli zikionekana kusimama..
 
Mchanganuzi wa maswala ya Biashara kutoka mjini Nakuru BW Antony Njagi anasema tangu serikali iruhusu bidhaa za kigeni za bei nafuu kuingizwa humu nchini ndipo wafanyikazi walianza kutaabika..
 
“Kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, Kenya imekuwa ikiendelea kuwataabisha raia wake huku ikiwatukuza raia wa kigeni kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara,” alisema.
 
Mazingira ya kufanya biashara humu nchini yanapozidi kuwa magumu huku wafanyibiashara wakitozwa kodi kubwa ikilinganishwa na biashara ndogo wanazofanya.
Kiwanda cha pareto kilikuwa kimefungwa kwa miaka mingi. Picha/ Richard Maosi
 Lakini anaona ni afadhali vyuo viache kufunzi kozi zinazohusiana na viwanda kwa sababu ya ukosefu wa ajira katika nyanja hizo.
 
Wasambazaji wa vifaa vya ujenzi Albhai Sharruf, Mache na C.K Patel pia walifunga huduma zao na kubakisha majengo ambayo yamebakia kuwa mahame.
 
Peter Ochieng aliyekuwa akifanya kazi katika silo za kuhifadhi nafaka anasema silo hizo zilikuwa zikiwasaidia wakulima kuhifadhi nafaka zao dhidi ya viwavi.
 
Anasema kabla ya kuhifadhi nafaka mkulima alitakiwa kuzikausha vizuri kisha akazisafirisha kwenye silo zinazozihifadhi.
Serikali ya Kaunti ya Nakuru imeanza kufufua kiwanda cha pareto. Picha/ Richard Maosi
 “Silo zilikuwa na jukumu kubwa la kuwatafutia wakulima soko ama kuzihifahi kwa muda ili ziwe salama,”alisema.
 
Lakini tangu silo zifungwe wakulima wengi walipata hasara huku baadhi yao wakikosa malipo yao kutokana na usimamizi mbaya .
 
Mpaka sasa wengi wao wamechoka kufuatilia malipo yao wakiamini kuwa pesa zao zilivujwa na watu wachache waliokuwa wakisimamia huduma za silo.
 
Ni kwa sababu hiyo kaunti ya Nakuru imeweka mikakati kadhaa ya kufufua viwanda hasa eneo la Viwandani ambapo ni maghala ya kuhifadhi nafaka.
Hii ni kampuni ya pareto iliyoanza tena kuendesha huduma baada ya Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui kuingilia kati. Picha/ Richard Maosi
 Gavana Lee Kinyanjui katika ajenda zake anaamini kuwa kwanza hatua hii ni lazima ianze na uboreshaji wa miundo msingi.
 
Alieleza Taifa dijitali kuwa pana haja kubwa kwa wawekezaji wa kibinafsi kuungana na wale wa umma ili kurejesha sifa na hadhi ya kaunti ya Nakuru.
 
“Kwa sababu ya ugatuzi sasa ni rahisi kurejesha nafasi nyingi za ajira kwa watu tukianzia na eneo la viwanda la Naivasha ambapo watu wengi wamekuwa wakitaabika kutokana na ukosefu wa viwanda,” akasema.
Haya ni yaliyokuwa majengo ya kampuni ya Bedrock Holdings iliyokuwa ikitoa huduma za ulinzi. Picha/ Richard Maosi
 Alieleza kuwa hivi karibuni Nakuru itapata hadhi ya kuwa jiji na hili litafungua njia kwa masoko ya nje hususan Afrika Mashariki.
 
Mradi wenyewe ameupatia jina la Kuziba Mwanya wa Uzalishaji kupitia Ajenda Nne Kuu ambapo anaamini uchumi wa kaunti utakua kwa asilimia 6.6 ifikapo 2022.

You can share this post!

Kampuni ya uchukuzi wa umma Thika Road yalaumiwa kwa...

Baadhi ya wadau vita dhidi ya dawa za kulevya walaumu...

adminleo