Akili MaliMakala

Wanahabari watunzaji mazingira watambuliwa

Na SAMMY WAWERU April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

BARA la Afrika linaendelea kuhangaishwa na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

Hayo, yanashuhudiwa licha ya Afrika kukadiriwa kuchangia chini ya asilimia nne ya athari hizo – utoaji wa gesi hatari aina ya Kaboni (Greenhouse gasses) ulimwenguni.

Viongozi na wadauhusika katika mazingira wakijikuna kichwa jinsi ya kupunguza athari hizo, ushirika wa wanaharakati kutetea haki za kibinadamu na vyombo vya habari, ndio – Consortium for Human Rights and Media (CHARM), umeibuka na mpango kutambua na kutuza wanahabari wanaoandaa habari na makala kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Mwaka huu, 2025, muungano huo kwa ushirikiano na

 Wits Centre for Journalism, Fojo Media Institute, na Magamba Network, uliandaa makala ya kwanza ambapo waandaaji wa taarifa za kidijitali kutoa hamasisho la mada lengwa, walipewa msaada wa kifedha (grants).

Mpango huo unajulikana kama Green Media Accelerator.

Aidha, wanahabari watano, akiwemo wakili mwanaharakati – walioibuka washindi, kila mmoja alituzwa kima cha Sh432, 000.

Waandishi hao wanatoka nchi za Kenya, Tanzania, Zimbabwe na Nigeria, wakiibuka kidedea kwenye orodha ya waliotuma maombi ya kupigwa jeki kuendeleza utunzi kutoka mataifa mbalimbali Afrika.

Mada zilizolengwa ni uhamasishaji mazingira, haki ya tabianchi, taarifa za upekuzi kulinda mazingira, ikiwa ni pamoja na hamasa kuhusu mbinu za kutunza mazingira na maliasili Barani Afrika.

Sally Ngoiri, Mkenya, ni miongoni mwa washindi walionufaika kupitia mpango huo.

Sally, mwanahabari mwenye tajiriba ya miaka saba huandaa makala (documentary) na filamu zinazohamasisha usafishaji mazingira na upanzi wa miti hususan maeneo kame.

Sally Ngoiri, Mkenya, anayefanya kazi na Kick Ass Films akionyesha cheti cha ushindi wa msaada wa fedha (grant) kupitia mpango wa Green Media Accelerator, aliopata mnamo Machi 28, 2025 katika hafla iliyoandaliwa Nairobi na Consortium for Human Rights and Media (CHARM). PICHA|HISANI

“Inasikitisha kuona jinsi mazingira yanaendelea kuharibiwa kwa utupaji taka kiholela haswa bidhaa za plastiki na ukataji miti. Hutumia makala na filamu, kwa njia ya kidijitali kuhamasisha umma haja ya kutunza mazingira,” Sally akaambia Akilimali.

Hafla ya kupiga msasa hoja za wanahabari waliorodheshwa washindi, ilifanyika kati ya Machi 26 hadi 28, 2025 katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nairobi.

Sally alidokeza kwamba huunda taarifa fupifupi ili kuteka vijana kupitia safu za mitandao ya kidijitali kama vile makundi ya kijamii WhatsApp, TikTok, Instagram, Facebook na X (awali Twitter).

Akilenga Nairobi, Machakos, Kajiado na Kiambu, mwanahabari huyu mchanga anasikitika Afrika inazidi kulemewa na athari za tabianchi, mazingira na kilimo kikiathirika pakubwa.

“Kando na kuhamasisha usafi wa mazingira, sharti turejeshe hadhi yake kwa kupanda miti. Taarifa ninazoandaa, mbali na kuzisambaza mitandaoni, huandaa hafla na umma kuhusu upanzi wa miti,” alielezea.

Aghalabu, kina mama ambao ni nguzo kuu kwenye jamii na watoto, ndio wanaathirika pakubwa kutokana na athari za tabianchi haswa maeneo kame.

Ashley Rudo Jim, mwanafilamu kutoka Zimbabwe, ambaye pia alitunukiwa, hutumia ujuzi wake kuhamasisha haki za kina mama na watoto.

“Huunda taarifa zinazoangazia changamoto zinazofika wanawake na watoto. Ikumbukwe, majanga kama njaa na ukame yanapotukia, wao ndio huathirika sana,” Ashley akasema.

Akiwa aliingilia taaluma ya uanahabari 2019, Ashley anafanya kazi na Matamba Film Labs for Women, Zimbabwe.

Huunda makala na filamu zinazoonyesha uhalisia wa mambo nyanjani kwa njia ya kidijitali, teknolojia ya kisasa ya AI, uhuishaji (animation) na pia picha ambazo huziunganisha kuwa makala.

Ashley anasisitiza haja ya wanawake na watoto kupewa kipaumbele kwenye kampeni dhidi ya athari za tabianchi, akiamini jitihada zao zitasaidia kuboresha mazingira hatua ambayo itakuwa na mchango mkubwa kupunguza makali ya kiangazi, ukame na njaa, vyote vikiwa kati ya ‘mazao’ ya mabadiliko ya tabianchi.

Mwanahabari mwingine mchanga aliyetambuliwa na kupokezwa msaada wa fedha ni Aurelio Mofuga kutoka Tanzania.

Mwanahabari Aurelio Mofuga kutoka Tanzania akionyesha cheti cha ushindi wa msaada wa fedha (grant) kupitia mpango wa Green Media Accelerator, aliopata mnamo Machi 28, 2025 katika hafla iliyoandaliwa Nairobi na Consortium for Human Rights and Media (CHARM). PICHA|HISANI

Akiegemea mfumo wa bunifu za kisasa, Aurelio, 27, ana mvuto kwenye teknolojia za kisasa kuangazia kuathirika kwa hewa na mazingira.

Hoja yake iliyomvunia ushindi, ilikuwa hamasisho si tu nchini Tanzania, bali pia Ukanda wa Afrika Mashariki na Bara la Afrika kuhusu ukumbatiaji magari yanayotumia nguvu za umma, hasa katika sekta ya uchukuzi wa umma.

“Matatu zilizopo barabarani zinazotumia kawi, idadi yake ni sawa na tone la maji baharini. Magari yanayotumia mafuta ya petroli na dizeli ndiyo mengi, na gesi ya Kaboni inayotolewa inachangia pakubwa kuharibu hewa,” Aurelio akasema, akisisitiza haja ya sekta ya uchukuzi kukumbatia magari yanayotumia nguvu za umeme.

Hoja yake ya mapenkezo ‘Daladala Verse nchini Tanzania’, iliangazia pakubwa mbinu kukabiliana na gesi za kijani kutoka kwenye magari na viwandani, mkondo anaotumia kutoa hamasa ukiwa ni makala, filamu, sanaa kwa njia ya michoro ya rangi na picha.

“Hutumia safu kama Instagram, Titktok, Facebook na X, na pia kutangamana na umma ana kwa ana.”

Ukosefu wa fedha kuboresha utendakazi, vifaa vya kisasa na mafunzo, ni kati ya changamoto ambazo hukumba waandishi wa habari.

Mkurugenzi wa Ubunifu katika shirika la Magamba Network, Samm Farai Monro, alisema uwekaji mikakati imara kupitia uwepo wa majukwaa kutambua jitihada za wanahabari wachanga na kuwapiga jeki kifedha, ni nguzo kuu kusaidia kuangazia athari hasi za mazingira.

“Tunapania kutumia mpango wa Green Media Accelerator kuwaunganisha na mianya ya ufanisi, watangamane na wataalamu na mashirika ya kuwasaidia, ili wafanikishe kampeni kurejesha hadhi ya Bara la Afrika,” akasema Farai.

Watano hao walioibuka washindi, kando na msaada wa fedha, watapitia mafunzo ya miezi sita ili wanolewe makali.

“Tunatumai mpango tulioanzisha utakuwa mfano kwa wengine kuandaa taarifa zenye mashiko,” akasema Dinesh Balliah, Mkurugenzi Wits Centre for Journalism.