WASONGA: Madaktari waliounganisha mkono wanafaa kutuzwa
Na CHARLES WASONGA
Kwa Muhtasari:
- Joseph Theuri alikimbizwa katika hospitali hiyo baada ya kukatwa mkono na mashine ya kusaga chakula
- Upasuaji uliodumu kwa saa 23 uliendeshwa na kundi la wataalamu 23
- Wataalamu hao wanafaa kujumuishwa kwenye orodha ya Wakenya ambao watapokea tuzo za kitaifa mwaka huu
- Wamedhihirishia ulimwengu kuwa hakuna haja kwa Wakenya kusafiri nje ya nchi kusaka huduma kama hizo
KWA mara nyingine, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) iliandikisha historia kwa kufanikiwa kuunga vipande vya mkono wa mwathiriwa aliyepelekwa humo kwa matibabu maalum.
Mgonjwa huyo, Joseph Theuri, 17, kutoka Kiambu, alikimbizwa katika hospitali hiyo baada ya kukatwa mkono na mashine ya kusaga chakula cha mifugo.
Upasuaji ulifanyawa na kundi la madaktari wakiongozwa na Catherina Kahiga na Ferdinand Nakole.
Itakumbukwa kuwa miaka miwili iliyopita (2016) madaktari wa KNH walifaulu kuwatengenisha pacha wawili waliokuwa wameshikana kiunoni.
Upasuaji huo uliodumu kwa saa 23 uliendeshwa na kundi la wataalamu 23 wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Shule ya Mafunzo ya Matibabu katika Chuo Kikuu cha Nairobi Prof Nimrod Mwangombe.
Kwa hakika wataalamu hawa wanafaa kutuzwa kwa kazi nzuri na kudhihirishia ulimwengu kwamba Kenya ina madaktari waliobebea si haba katika upasuaji.
Wataalamu hao wanafaa kujumuishwa kwenye orodha ya Wakenya ambao watapokea tuzo za kitaifa mwaka huu, kwa machango wao katika kuboresha maisha ya wanajamii na Wakenya kwa jumla.
Ni aibu kuwa Profesa Mwangombe na wenzake, walifanikisha upasuaji uliwatenganisha watoto hao wa kike kwa majina, Blessing na Favour, hawakuwa miongoni mwa Wakenya 54 waliopokea tuzo hizo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017.
Badala yake orodha hiyo ilijaa watu ambao mchango wao kwa jamii ni wa kutiliwa shaka kama vile Bw Martin Kamotho, al maarufu “Githeri Man”.
Ufanisi ambao umeandikishwa na madaktari wa KNH, hasa katika nyanja ya upasuaji, unafaa kuisukuma serikali kuwekeza hela nyingi katika ununuzi wa vifaa vya kisasa katika taasisi hiyo na na hospitali zingine za ngazi ya kaunti.
Hii ni kwa sababu wataalamu hao wamedhihirishia ulimwengu kuwa hamna haja kwa Wakenya kusafiri nje ya Kenya kusaka huduma kama hizo kuwa wana uwezo na ujuzi wa kutoa huduma hizo humu nchini na kwa bei nafuu.
Lakini sharti vifaa maalum na mazingira faafu ya utendakazi, kando na motisha uwepo. Naamini kuwa Kenya ina uwezo wa kutibu magonjwa mengine sugu kama saratani, kisukari na maradhi ya moyo.