• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
WASONGA: Ruto anapopinga nyadhifa zaidi, apinge pia ‘ikulu’ yake

WASONGA: Ruto anapopinga nyadhifa zaidi, apinge pia ‘ikulu’ yake

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amekuwa akijinadi kama kiongozi anayeweka mbele maslahi ya Wakenya wa kawaida, kwa sababu alizaliwa katika familia maskini.

Yamkini katika ujana wake aliwahi kuwa mchuuzi wa kuku katika eneo la Kamagut, Kaunti ya Uasin Gishu.

Na hivi majuzi alirejea huko ambapo aliongozwa mnada wa kuku uliozalisha jumla ya Sh6 milioni kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wa ndege hao.

Hii ndiyo maana, nadhani, anapinga shinikizo za kuifanyia katiba ya sasa marekebisho kwa lengo la kubuniwa nyadhifa zaidi za uongozi katika safu ya juu serikalini.

Amekuwa akishikilia kuwa kura ya maamuzi ya kufanikisha mpango huo, itagharimu pesa nyingi ambazo zinapaswa kuelekezwe katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa Wakenya wote.

Lakini kinaya ni kwamba Bw Ruto amenyamaza kuhusu mpango wa kumjengea ‘Ikulu’ ndogo mjini Mombasa. Awamu ya kwanza ya mpango huo itagharimu Sh50 milioni. Kulingana na bajeti ya ziada iliyowasilishwa bungeni Alhamisi wiki jana, itaanza hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kimani Ichung’wa aliwaambia wabunge kwamba pesa nyingine zaidi zitatengewa mradi huo kwenye bajeti ya mwaka ujao wa kifedha wa 2018/19 unaoanza Julai 1.

Hii ina maana kuwa mradi huo utagharimu pesa nyingi zaidi. Kwa maoni yangu, mradi huu sio wa dharura sasa ambapo Wakenya wengi wanaathirika na mafuriko yanayosabibishwa na mvua ya masika inayoshuhudiwa kote nchini.

Vile vile, sioni dharura katika mpango wa Bima ya Matibabu kwa Wanafunzi wa Shule za Upili itakayogharimu mlipa ushuru Sh4.8 bilioni. Sisemi kuwa mpango huu ni mbaya, la hasha! Tasnifu yangu ni kwamba sio mpango wa dharura wakati huu.

Kwa maoni yangu, wakati huu serikali inapasa kuelekeza fedha nyingi katika mpango wa kuwasaidia Wakenya walioathirika na mafuriko pamoja na mpango wa upanzi wa miti ili kuimarisha viwango vya misitu nchini.

Bajeti ya ziada ambayo itajadiliwa bungeni Jumatano wiki hii inafaa kutenga pesa za kukarabati madarasa ambayo yaliharibiwa na mvua katika shule kadhaa humu nchini wala sio pesa za kujenga “Ikulu” ya Naibu Rais ni mipango mingine ambayo sio ya dharura.

Huenda baadhi ya shule maeneo ya Tana River, Baringo na Kisumu zikakosa kufunguliwa Jumatano kwa sababu madarasa yaliharibiwa na mafuriko Namtaka Bw Ruto kuamuru kusitishwa kwa mradi huo mara moja na pesa hizo zielekezwe katika mipango ya kuwasaidia wahanga wa mafuriko.

You can share this post!

King’asti aelezea alivyomhepa mumewe baa na kumlisha...

Makahaba 1,000 tayari kuandamana uchi iwapo Conte...

adminleo