Michezo

Malkia Strikers watakaowania tiketi ya kushiriki All-African Games watajwa

May 5th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) limetaja kikosi cha wachezaji 19 kuanza mazoezi mara moja kwa makala ya 12 ya mashindano ya ukanda wa tano ya kufuzu kushiriki michezo ya African Games itakayoandaliwa jijini Kampala nchini Uganda mnamo Mei 18-25.

Timu hiyo ni mchanganyiko wa wachezaji wazoefu na chipukizi. Itanolewa na kocha mkuu wa klabu ya KCB Japheth Munala, ambaye pia ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanawake almaarufu Malkia Strikers. Atasaidiwa na kocha mkuu wa klabu ya wanawake ya Prisons, Josp Barasa.

Kikosi hiki ambacho kinajumuisha mastaa kama Mercy Moim, Jane Wacu, Noel Murambi na seta mzoefu sana Janet Wanja, kilichaguliwa na kamati ya makocha ya KVF baada ya kukamilika kwa shindano la Gavana wa kaunti ya Kitui wikendi iliyopita na kutangaziwa kwa umma Mei 3.

Kenya ndio mabingwa watetezi wa mashindano ya African Games baada ya kunyakua taji hili kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999 katika makala yaliyopita mwaka 2015 jijini Brazzaville nchini Congo. Walichabanga Cameroon kwa seti 3-1 katika fainali.

Malkia Strikers inashikilia rekodi ya mataji mengi ya voliboli ya wanawake ya African Games baada ya kutawala makala ya mwaka 1991, 1995, 1999 na 2015.

Kikosi cha Malkia Strikers:

Washambuliaji wa pembeni kushoto

1. Mercy Moim (Prisons)

2. Pamela Masaisai (Prisons)

3. Sharon Chepchumba (Pipeline)

4. Noel Marambi (KCB)

5. Leonida Kasaya (KCB)

Wazuiaji wa katikati

6. Edith Wisa (Prisons)

7. Trizah Atika (Pipeline)

8. Gladys Ekaru (Pipeline)

9. Jemima Siangu (KCB)

10. Caroline Sirengo (DCI)

11. Lorine Chebet (KCB)

Washambuliaji wa pembeni kulia

12. Emmaculate Chemtai (Prisons)

13. Violet Makuto (KCB)

Maseta

14. Janet Wanja (Pipeline)

15. Jane Wacu (Prisons)

16. Esther Mutinda (Pipeline)

17. Joy Luseneka (Prisons)

Malibero

18. Elizabeth Wanyama (Prisons)

19. Linzy Cheruto (KCB)

20. Agripina Kundu (Pipeline)