Maoni

MAONI: Gen Z wakishamaliza na Ruto wakabili magavana


VIJANA barobaro, almaarufu wa Gen Z, wamekuwa wakimpa presha Rais William Ruto wakimtaka kutimua mawaziri wote wakisisitiza kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao na baadhi yao wanaogelea kwenye sakata za ufisadi.

Rais Ruto, angali anajikokota kuvunja baraza la mawaziri na kuwaelezea Wakenya mikakati yake ya kupambana na ufisadi serikalini.

Wito wa kumtaka Rais Ruto avunje baraza lake la mawaziri ni ishara kwamba Wakenya wamepoteza imani na utendakazi wa serikali na Kiongozi wa Nchi hana budi kuanza upya kwa kuteua mawaziri wapya.

Ufisadi umesalia kuwa donda sugu ambalo limelemaza uchumi wa nchi kwa miaka na mikaka.

Tangu Rais Ruto kutwaa hatamu ya uongozi wa nchi, ufisadi umeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Ripoti kuhusu hali ya ufisadi iliyotolewa Septemba mwaka jana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), inaonyesha kuwa wastani wa kiwango cha fedha zinazotolewa kama hongo humu nchini kiliongezeka maradufu kutoka Sh6,865 mnamo 2022, hadi Sh11,625 mwaka jana.

Jumba Kuu la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC). PICHA| HISANI

Kwa mujibu wa EACC, Wakenya wanaotaka ajira katika serikali kuu wanahitajika kulipa hongo isiyopungua Sh163,260!

Hii inamaanisha kuwa ukiwa na hongo ya Sh10,000 ni vigumu kupata huduma! Nchi inanuka ufisadi. Ufisadi ni sumu kwa vizazi vijavyo na hiyo ndiyo maana Gen Z wanataka Rais Ruto aonyesha juhudi za kukabiliana na zimwi hilo kabla liangamize nchi.

Japo jukumu la kupambana na ufisadi ni la EACC, Kiongozi wa Nchi ana uwezo mkubwa wa kupambana nao kwa kutimua mawaziri na maafisa wengine serikalini wanaojipata kwenye sakata za wizi wa mali ya umma.

Baada ya kumaliza mapambano dhidi ya Rais Ruto, vijana wa Gen Z waanze kupambana na serikali za kaunti ambazo zimejaa uvundo wa ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na ajira zinazopendelea jamaa za magavana na maafisa wenye ushawishi serikalini.

Ripoti ya EACC, kwa mfano ilionyesha kuwa kiasi cha hongo inayotolewa katika Kaunti ya Pokot Magharibi ni Sh56,695, Nairobi (Sh 37,768); Murang’a (Sh 18,378); Kisii (Sh 16,810); Uasin Gishu (Sh 11,136) miongoni mwa kaunti nyinginezo. Ni aibu kwamba serikali za kaunti zimejaa wafanyakazi ambao ni jamaa za magavana, mawaziri au maafisa wakuu serikalini.

Ufujaji wa fedha za umma katika serikali za kaunti umekita mizizi.

Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o ilionyesha kuwa serikali za kaunti zilitumia jumla ya Sh3 bilioni ndani ya miezi mitatu kati ya Julai na Septemba 2023 katika shughuli zisizonufaisha wananchi kama vile safari za ndani na nje ya nchi.

Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o. PICHA| HISANI

Kaunti ya Migori, kwa mfano, ilitumia Sh184 milioni katika safari za ndani na nje ya Kenya.

Ufujaji wa fedha za umma wa aina hii ni usaliti kwa mfumo wa ugatuzi na kizazi kijacho.