Kwani Kenya ni jukwaa la ‘vipindi’ hatari?
NINA rafiki ambaye hunicheka nikishangilia mchezo wa kandanda, na nikimuuliza sababu ya kunicheka ananicheka zaidi.
Tabia yake hiyo hainiudhi, hunisababishia kicheko zaidi, sote wawili tukajipata tukiangua kweli-kweli!
Aliwahi kunieleza eti alipoteza imani na mchezo huo alipogundua kuwa ni ‘kipindi’ kinachoandaliwa na wasimamizi kwa ajili ya kuendeleza biashara.
Anaamini hata matokeo ya mechi zote hupangwa tangu mwanzo kwa mapenzi ya wafadhili, yaani zile kampuni kubwa-kubwa zilizo na biashara ambazo hutokea kwenye runinga mechi zikiendelea.
Yeye ni shabiki sugu wa raga, sikwambii na mkufunzi pia. Ananieleza kuwa raga haina wakora kwa sababu haijawa maarufu sana duniani.
Katika nchi ambapo takriban kila kitu hupangiwa nyuma ya pazia kabla hakijatokea jukwaani, huwezi kupuuza mtizamo wa rafiki yangu, si kuhusu kandanda tu bali pia mambo mengi
Najiuliza iwapo Kenya ni jukwaa kubwa ambapo kila mtu anafanya ‘kipindi’ chake kwenye kona yake kana kwamba wengine hatupo kabisa.
Hivi ni kwa vishawishi vya aina gani ambapo ukora wa kupenyeza wajanja kwenye mahojiano ya taasisi muhimu kama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) unaweza kutokea?
Nusra nikimbie mahakamani kushtaki utundu huo, lakini nimekumbuka kuwa hiyo ndiyo hulka ya taifa letu. Tunaingiza mchezo wa mjini katika kila kitu, hata elimu.
Hivi umewahi kujiuliza mzazi anayemsaidia mwanawe kuiba mtihani huwa amechomekwa mzizi na waganguzi wa kwao wakashindwa kumgangua, au unamvulia kofia kwa kufaulu ujanja?
Mwanafunzi anayesaidiwa kuiba mtihani, akapata alama ya ‘A’ na kuishia kusomea udaktari au uhandisi, ambako pia anasaidiwa kupita mitihani, ni salama kukutibu au kukujengea nyumba?
Si siri kwamba, ukiwa mwalimu, baadhi ya matajiri na watu mashuhuri watakuletea wanao, wakununulie ‘chai’ ya mfukoni au ya M-Pesa, ukiwa hafifu upokee na kutabasamu kijinga, wakiondoka wakuonye: “Na asianguke mtihani wowote!”
Katika mazingira hayo, unaona ajabu gani ikitokea kwamba baadhi ya wagonjwa nchini wana maisha ya wiki moja kama nzi, nayo majumba makubwa hujiangukia ovyo yakitaka?
Na kwa kuwa hata nao baadhi ya wapelelezi na wachunguzi wetu wengineo walipitia milango ya nyuma wakielekea vyuoni kusomea taaluma hiyo, wao pia hawajui wachunguze nini.
Wachache walio na maadili wanazidiwa nguvu na wengi wasiojua kwa nini wako mahali pale, kwa sababu kikawaida vijito hujiunga na mito, nayo mito ikaingia baharini.
Angalia orodha hii ya waliopenyezwa IEBC hata baada ya kushindwa katika usaili, uniambie unaona nini – Noor Hassan Noor, Jibril Maalim Mohammed, Michael Ben Oliewo, Charles Kipyegon Mutai, Stephen Kibet Ng’eno na Joel Mwita Daniel.
Ukora mwingi tunao, na tunafurahia unapotunufaisha, lakini sharti tukumbuke busara za wazee wangu kwamba ujanja wa nyani huishia jangwani. Ipo siku!