Maoni

MAONI: Arati, Nassir wanamhadaa Raila kwamba ana nafasi ya kugombea urais 2027

Na CECIL ODONGO August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PENDEKEZO la baadhi ya wanasiasa wa ODM kuwa kinara wao Raila Odinga awanie urais mnamo 2027 ni hadaa tu ili wamtumie kupata nyadhifa zao.

Kwa sasa juhudi zote zinastahili kuelekezwa kwa kampeni ya Bw Odinga kunasa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), badala ya kushiriki siasa za 2027.

Mwishoni mwa wiki jana, Gavana Simba Arati wa Kisii na mwenzake wa Mombasa, Abdulswamad Sheriff Nassir, walidokeza kuwa Bw Odinga bado anatosha kuwania urais katika uchaguzi wa 2027.

MaBw Arati na Nassir waliteuliwa kama manaibu viongozi wa Bw Odinga katika ODM, baada ya ycliffe Oparanya na Hassan Joho kujiuzulu ili kutwaa nafasi za uwaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.

Kabla ya uteuzi huo, Bw Arati alikuwa akihudumu kama naibu mwenyekiti wa ODM, japo Bw Nassir hakuwa na wadhifa wowote chamani kando na kuwa jemedari halisi wa Bw Odinga.

Mwanzo, magavana hawa wawili wafahamu kuwa kinara huyo wa upinzani kwa sasa anaelekea kupoteza umaarufu hasa miongoni mwa kizazi cha sasa cha vijana, Gen Z, ambacho kinamlaumu kwa kusambaratisha mchakato wao wa mageuzi.

Gen Z walikuwa wakiendeleza maasi ya kubandua utawala wa Rais William Ruto, lakini ni dhahiri yamefifia baada ya Bw Odinga kuanzisha ushirikiano na Rais.

Iwapo vijana watachukua kura kwa wingi na 2027 waamue kuondoa wanasiasa wakongwe na wale wanaohisi wameshindwa kustawisha taifa, basi Bw Odinga na Rais Ruto hawatakuwa na lao.

Kuwaambia Wakenya kwamba ODM haishirikiani kivyovyote na utawala wa sasa ni hadaa tupu.

Itakumbukwa kuwa Bw Odinga alipinga vikali uteuzi wa marehemu Joseph Nkaissery kwenye Baraza la Mawaziri la utawala wa Jubilee mnamo Desemba 2014.

Wakati huo alisema hatua ya kuteua wabunge au viongozi wa upinzani ililenga kulemaza upinzani ili usitekeleze wajibu wake kuiweka serikali kwenye darubini.

Sasa kipi kimebadilika kiasi cha yeye kusema amekodisha wandani wake walioteuliwa mawaziri serikali eti wasaidie kuokoa chombo cha Kenya Kwanza kilichokuwa kikizama?

Pili, Bw Odinga atakuwa ametimu miaka 82 na japo urais hauna kigezo cha umri, ujana umempa kisogo na mwili hautakuwa na nguvu za kustahimili kukurukakara za kupiga kampeni na kisha kuongoza taifa; heri aunge mkono mgombea mwingine atakayemrithi.

Kigogo huyo wa kisiasa ameshindwa urais mara tano; mara nne kati yazo amesisitizia wafuasi wake kuwa alichezewa shere.

Mara nyingi wanasiasa wametumia jina la ‘baba’ kupata viti lakini yeye anashindwa. Hii ni mbinu nyingine ambayo sasa inatumiwa na magavana Arati na Nassir.

Bw Odinga asipowahi kiti cha AUC asiwanie urais Kenya bali apishe mwaniaji mwingine. Kama hana kismati kuwa rais hata akiwania 2027 bado hatashinda.

Wawili hawa wanajua kuwa ODM itakuwa imara tu kama Raila yupo debeni huku nao wakilenga kuhifadhi viti vyao vya ugavana. Wanajua kuwa ODM isipokuwa imara na Raila akiwa AUC basi wanaweza kushindwa kupata muhula wa pili.

Kile Raila anastahili kufanya ni kumakinikia kampeni ashinde AUC ili ahudumu kwa miaka minne na akiona kuwa bado yupo ngangari atetee wadhifa huo mnamo 2028.

Asipowahi kiti cha AUC basi asiwanie urais bali apishe mwaniaji mwengine ambaye atazingatia maslahi ya ngome zake za kisiasa. Kama hakuandikiwa urais hata akiwania 2027 bado hataupata.

Mnamo 2027 asiwanie urais bali atumie ushawishi wake kuunga mkono mrengo utakaoshinda kwa sababu ni wazi kivyovyote vila yeye huishia kuwa serikalini baada ya uchaguzi.