Maoni

MAONI: Hivi demokrasia iliyokufa Tanzania, itafufuka lini?

Na DOUGLAS MUTUA September 26th, 2024 3 min read

JUZI nimecheka kidogo baada ya kuona video ya mzee wa Kitanzania akieleza jinsi rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, alivyorejelea wananchi wa mataifa matatu ya Afrika Mashariki: Kenya, Uganda na Tanzania.

Kwa mujibu wa Mtanzania huyo, Mzee Kenyatta alisema Wakenya ni sawa na watu waliolala, ambao wanaweza kuamka na kudai haki zao; Waganda ni wagonjwa, hivyo wakipona watadai haki zao; ila Watanzania ni wafu wasioweza kamwe kudai haki zao.

Masikioni hiki kinasikika kama kichekesho, lakini ukitafakari sana kisha uangalie mambo yanavyokwenda katika mataifa hayo, utakubaliana na mtazamo huo.

Si siri kwamba Wakenya ni wajuaji wakali wanaomkabili yeyote, hasa aliye madarakani, hivyo haikosi viongozi wetu huishi kwa hofu kwamba huenda siku moja tukaamka na kuwavaa wazima-wazima, kwa wingi wa mikono yetu tuchukue wanachotunyima.

Ni wazi kwamba Waganda walipona kitambo sana kwa kuwa, japo wamekaliwa mguu wa kausha na dikteta mkongwe, Yoweri Kaguta Museveni, wamemjulisha kuwa hawamtaki, akiondoka leo hii watashangilia. Wamejaribu kumng’oa madarakani akanata!

Hali ni tofauti kabisa unapowaza kuwahusu ndugu zetu Watanzania. Hakika wale ni wafu kidemokrasia, wanaiogopa serikali kama moto na wanatoa visingizio vya kupenda amani kuliko haki, wakitaka kuandamana kisha watishiwe hatoki mtu ndani!

Kuwapa au kuwanyima haki ni uamuzi wa rais wao, na aghalabu huwanyima kuliko kuwapa. Akiwaruhusu kidogo kufoka, wanasema mambo ambayo yanamkera kiasi cha kughairi nia ya kuwapa haki.

Kisha? Analaumiwa na makada wa ngazi za juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala, ambao tangu hapo wamezoea vya kunyonga, vya kuchinja hawajui, mwishowe anajilaumu kwa kuwapa uhuru wa kumtukana, tena anaapa watamkoma.

Hivi Watanzania walimruhusuje mtu mmoja kuwapa au kuwanyima haki ambazo kila mtu huzaliwa nazo? Wanataka kuishi hivi hadi lini?

Watakwambia wazi kwamba tatizo ni Katiba kandamizi waliyoonywa na Mwalimu Julius Nyerere kwamba inampa rais mamlaka ya nduli, ila hawafanyi chochote kuifanyia mabadiliko.

Wanasubiri muujiza utoke mbinguni, uchaguzi wa mwakani uwe huru na wa haki, yaani mambo yawaendee vyema tu bila kuyakatia jasho.

Ukikutana nao waambie hilo halifanyiki hata katika ulimwengu wa kusadikika. Lazima wafurukute. Lazima wapigwe na kuumizwa wakitetea haki zao. Serikali haikupi chochote bila kuitikisa na kuifikicha.

Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wakithubutu kuiga mambo yanayofanyika Kenya, kama vile kushiriki maandamano ya amani, wanakamatwa hata kabla hawajatoka nyumbani kwao.

Hayo yaliwatendekea viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); Mwenyekiti Freeman Mbowe na Naibu Mwenyekiti Tundu Lissu, Jumatatu iliyopita.

Wawili hao walinuia kujiunga na maandamano ya amani yaliyopangwa kwa ajili ya kupinga visa vya utekaji nyara na mauaji ya Watanzania wanaoikosoa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Serikali iliwakamata wanasiasa hao na wafuasi wao mwezi uliopita kwa tuhuma kwamba wanaongoza wananchi kuikabili kutokana na ukandamizaji wake.

Ijapokuwa Mzee Kenyatta aliwahukumu vikali Watanzania kwa kuwaita wafu, matukio ya watu kuikosoa serikali wakaishia kutiwa ndani na hata kuuawa ni ishara kwamba ufufuo wa kisiasa umeanza kutokea.

Watanzania, japo kwa kasi ya kobe, wameanza kujitambua na kuzifahamu haki zao. Wameanza kuzidai na hawatapumzika mpaka wazipate.

Wanaona mambo yanavyoendelea duniani, hata kwa jirani yao Kenya na wametamani neema ziwashukie na wao, waishi bila mijeledi ya mkoloni mweusi anayezungumza Kiswahili kwa ufasaha wa kupigiwa mfano kama wao. Kuonjeshwa kubaya eti.

Ajabu akidi ni kwamba wasioonekana kuwa na mwao na mabadiliko hayo ni viongozi walio madarakani, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kufumaniwa na mageuzi ya kisiasa wakiwa katika usingizi wa pono usiojua wakati wa kuamka.

Kwa kawaida, mabadiliko ya kisiasa yakianza huwa hayazuiliki. Hata yakifanyika polepole namna gani, hatimaye malengo yake huafikiwa kwa vyovyote vile, katika mazingira rafiki au vinginevyo.

Na kwa kuwa mabadiliko hayo hayamtegemei mtu mmoja, hata wanaoyaanzisha wakiuawa kwa sababu za kisiasa au kwenda mbele ya haki kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu, nafasi zao huchukuliwa na wengine na harakati kuendelea.

Mabadiliko ya kisiasa yalipoanza kutokea nchini Kenya miaka ya themanini, marehemu Rais Daniel Moi aliyapinga kwa kuwatowesha na kuwaua wengi, akayahujumu kiuchumi baadhi ya maeneo yaliyompinga, lakini hakufaulu katika uovu wake huo.

Aliondoka madarakani, na Mungu akamweka hai kwa karibu miaka 20, akashuhudia nchi ikitawaliwa kwa njia bora zaidi na watu alionuia kuangamiza. Kumbe alikuwa mwoga tu, nao alioogopa walikuwa wazalendo wa kweli?

Anachopaswa kukielewa Rais Samia na wenzake wa CCM ni kwamba Tanzania ni ya Watanzania wote, hata hao wanaokamatwa kwa raha zao, hivyo kila mmoja ana haki ya kutoa maoni kuhusu anavyotaka kuongozwa.

Fikra zao kwamba CCM ina ukiritimba wa maarifa ya kuiongoza nchi zinaweza tu kushikiliwa na mtu asiyeweza kuunga moja na moja akapata mbili, mbumbumbu mzungu wa reli hasa! Woga wao hauifai kitu Tanzania, unaihini.

[email protected]