Maoni

MAONI: Salasya hatoshi unga kubishana na Raila

Na CECIL ODONGO March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya anastahili kukoma kupimana ubabe na kumpiga vita Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa sababu atalemewa na ndio ataumia zaidi.

Bw Salasya alinyoroshwa vizuri katika uga wa Nyayo na mashabiki wa soka wikendi.

Waliomtia adabu walisikika wakisema anastahili kumheshimu Raila na Rais William Ruto na wamekerwa na ukosoaji wake mitandaoni kwa viongozi hao.

Mwanzo, nalaani ghasia ambazo zilimkumba Bw Salasya ambaye amekuwa na mdomo wembe kiasi kuwa huwezi kufikiria ni kiongozi mwenye hadhi ya ubunge.

Si vyema kwa watu kujitokeza tu na kumpiga mbunge jinsi ambayo Bw Salasya alipigwa, ikiwemo kurushiwa tangi. Kipigo hicho hakikufaa wala si vyema kusherekewa kwa sababu tu ya tofauti za kisiasa.

Hata kama wananchi wana machungu kivipi na viongozi ambao wana mtazamo tofauti nao vigogo wao wa kisiasa, hawafai kuwapiga kwa kuwa Kenya ni taifa la kidemokrasia.

Pengine mbunge huyo angefahamu kuwa machapisho yake mitandaoni ya kukosoa Raila na Rais yangemweka pabaya na wafuasi wao asingefika Nyayo.

Hata hivyo, mbunge huyo naye anastahili kuchunga ulimi wake na kukoma kutumia mitandao vibaya kuwatusi viongozi wengine na amakinikie utendakazi wa kuridhisha kwenye eneobunge lake.

Mwanzo, lilikuwa tukio baya zaidi kwa Bw Salasya kumkejeli Bw Odinga baada ya kupoteza kura ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mwezi uliopita.

Kwenye video iliyosambaa baada ya kura hiyo, mbunge huyo wa DAP-Kenya alimtaka Raila astaafu siasa akisema ana tamaa ndiposa aliwasaliti vijana waliokuwa na mageuzi.

Hakika lugha aliyotumia Bw Salasya kwenye video hiyo haikufaa hata kidogo kwa sababu Bw Odinga, 80, ni kiongozi ambaye amepigania mageuzi nchini wala hakuna ushahidi wowote kuwa alisaliti Gen Z na kutumia maasi yao kujinufaisha kisiasa.

Gen Z bado wapo wala Raila hakuwashika miguu au kuwazuia kuandamana ila aliwaambia tu washiriki mdahalo kusuluhisha malalamishi yao.

Bw Salasya, 36, bado ni kijana na anaweza kuwaongoza wengine waandamane iwapo anaona bado serikali inawatesa vijana.

Aidha, Salasya haiwezekani tu ni kuwa yeye ndiye hupigwa kila siku katika mikutano.

Mnamo Machi 10 alivamia mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Rashid Echesa kisha akaanza kumzomea tukio ambalo halikufaa.

Mara si moja amepigwa katika eneobunge lake na pia amevamia mikutano ya wanasiasa wengine akizua ghasia. Kwani yeye ni spesheli aje awadhuru wengine na atarajie wanyamaze tu wasimlipizie?

Huyu Bw Salasya ndiye kiongozi atapachika video mtandaoni na kujianika akivuta bangi? Yaani hakuna mazuri anayoweza kuhusishwa naye ila tu ni fujo.

Anapodai kuwa ni Waluo ndio walimpiga Jumapili (Machi 23, 2025), alijua aje ni wahuni hao walitoka kabila hilo ilhali hata kwao amewahi kunyoroshwa na hakutaja jina la kabila lake?

Kile ambacho, Bw Salasya anastahili kuwa nayo ni nidhamu, ajirekebishe na amwombe Raila na viongozi wengine msamaha ili amakinikie kazi yake ya ubunge.

Kuanza vita na Raila ni kupoteza hata kabla vita vyenyewe vianze. Huyu ni kiongozi ambaye ana ufuasi mkubwa na hata marais waliowahi jaribu kumkata miguu kisiasa walinywea na kuanza kufanya kazi naye.

Bw Salasya hawezani na Raila kisiasa na kama ameamua kuchukua mwelekeo tofoauti kisiasa, basi aendeleze siasa zake kisheshima.