Habari Mseto

Mbunge Kuria Kimani: Msiwe na wasiwasi, tutapiga msasa kabisa mawaziri walioteuliwa

Na JOHN NJOROGE July 21st, 2024 1 min read

MBUNGE wa Molo Kuria Kimani amewahakikishia Wakenya kuwa watapiga msasa ipasavyo mawaziri walioteuliwa ili kuipa nchi baraza la mawaziwi wenye uwezo na waliohitimu ambao watapeleka taifa mbele kwa kumsaidia Rais William Ruto kutekeleza majukumu yake.

Mbunge huyo alisifia uteuzi uliofanywa akisema kwa mara ya kwanza Rais ameteua vijana katika baraza lake jipya la mawaziri.

Akihutubia mamia ya wafuasi wake katika uwanja wa Mariashoni alipojitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu makazi yake na magari kuharibiwa na bidhaa za thamani isiyojulikana kuporwa wakati wa maandamano dhidi ya serikali, Kuria aliwataka wakazi hao kumuunga mkono na kumuombea rais anapoendelea kutekeleza majukumu yake.

“Namshukuru Rais kwa kuwasikiliza wananchi wake kwa kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 na kupunguza bajeti hadi kufikia kiwango kilichowekwa, mjadala unaoendelea ni kuhusu bajeti ya nyongeza bungeni,” alisema mbunge huyo, akiongeza kuwa baadhi ya watu walieneza hmbazo anasema hazikuwa kweli kuhusu mswada huo.

Alisema katika katiba ya Kenya, rais aliye madarakani anaweza tu kuondolewa kwenye kiti hicho kupitia kwa kura hivyo akawataka wanaosema kuwa rais aondoke madarakani, kusubiri hadi Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Alibainisha kuwa ikiwa rais atajiuzulu, nafasi yake inaweza tu kuchukuliwa na naibu wake.

Aliwataka vijana kujiandikisha kuwa wapiga kura na kujitokeza kwa wingi pindi uchaguzi ukifika ili kuwapigia kura viongozi wanaowataka.

Mbunge huyo alisema kuwa hawataruhusu mtu yeyote kuharibu mali kwa manufaa yao binafsi akitolea mfano tukio ambapo nyumba yake iliharibiwa na kuporwa, magari kuchomwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.

Alikemea tukio hilo na kutaka kuwepo kwa amani na kuongeza kuwa baadhi ya watu walikuwa wakitafuta damu ya wabunge wakati wa tukio hilo la kupinga mswada huo wa fedha.

[email protected]