Michezo

Everton yapata uhai, Saints waonja ushindi Liverpool ikiimarisha rekodi ya kutoshindwa

February 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

EVERTON waliendelea kujiweka salama kabisa katika vita vya kuepuka shoka la kushushwa daraja baada ya kubwaga Leicester 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Jumamosi.

Mabao hayo yalitiwa kimiani na Norberto Bercique Gomes Betuncal anayefahamika kama Beto (mawili), Abdoulaye Doucoure na Iliman Ndiaye ugani Goodison Park.

Nao Bournemouth walishuhudia rekodi yao ya kutoshindwa michuano 11 ikivunjiliwa mbali baada ya kuchapwa 2-0 na viongozi Liverpool, ambao wameimarisha rekodi ya kutopoteza hadi mechi 19.

Wenyeji Bournemouth, waliofyeka Nottingham Forest 5-0 Januari 25, walipoteza nafasi nzuri za Justin Kluivert na Antoine Semenyo kabla kujipata chini 1-0 kupitia penalti ya Mohamed Salah iliyopatikana baada ya beki Lewis Cook kuangusha mvamizi Cody Gakpo ndani ya kisanduku katika uwanja wa Vitality.

Mohamed Salah wa Liverpool avurumisha shuti iliyompita mchezaji wa Bournemouth na kutumbukiza wavuni kufunga bao la pili. PICHA | REUTERS

Salah alipachika bao la pili baada ya Curtis Jones kupokonya Justin Kluivert mpira, akapasiana vyema na Darwin Nunez na Luis Diaz kabla kummegea mshambulizi huyo wa Misri ambaye sasa ana magoli 21 msimu huu.

Majirani wa Liverpool, Everton nao waliendelea kujiweka salama kabisa katika vita vya kuangukiwa na shoka baada ya kubwaga Leicester 4-0 kupitia mabao mawili ya Norberto Bercique Gomes Betuncal anayefahamika kama Beto, pamoja na moja moja kutoka kwa Abdoulaye Doucoure na Iliman Ndiaye ugani Goodison Park.

Newcastle walikubali kipigo cha 2-1 kutoka kwa wageni Fulham ugani St James’ Park. Jacob Murphy aliweka waajiri wake kifua mbele dakika ya 37 kabla ya Newcastle kuruhusu Fulham kupata mabao kutoka kwa Raul Jimenez na Rodrigo na kuwaduwaza nyumbani kwa mara ya kwanza katika mechi tisa.

Nao Southampton walimaliza ukame wa mechi 13 bila ushindi ligini kwa kuchabanga wageni Ipswich Town 2-1 kupitia mabao ya Joe Aribo na Paul Onuachu. Aribo alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 21, lakini Liam Delap akasawazisha dakika 10 baadaye. Onuachu alihakikishia Saints alama tatu kwa kufuma wavuni bao la pili dakika ya 87.

Baada ya kusakata mechi ya 23, Liverpool ya kocha Arne Slot inaongoza kwa alama 56, tisa mbele ya nambari mbili Arsenal. Nambari tatu Nottingham Forest pia ina pointi 47, lakini imesakata mechi 24.

Wachezaji wa Southampton baada ya kufunga bao dhidi ya Ipswich Town. PICHA | REUTERS

Mabingwa watetezi Manchester City wanapatikana katika nafasi ya nne kwa alama 41 nao Newcastle wanafunga tano-bora kwa 41. Chelsea na Bournemouth wamekusanya alama 40 kila mmoja katika nafasi ya sita na saba, mtawalia. City na Arsenal watavaana katika mchuano wao wa 24 hapo Jumapili.

Nambari 15 Everton sasa wako alama 10 nje ya mduara hatari wa kutemwa tangu waajiri tena kocha David Moyes. Wamezoa alama 26, mbili mbele ya nambari 16 Tottenham nao Leicester ni nambari 17 kwa alama 17.

Wolves na Ipswich wana alama 16 kila mmoja nao Southampton wanavuta mkia wakiwa na pointi tisa. Timu tatu za mwisho ziko katika mduara hatari wa kushushwa ngazi.