Harambee Stars yaumwa na simba wa Cameroon huko Yaounde
HARAMBEE Stars ya Kenya imedondosha alama zote tatu kwenye mechi yake ya tatu ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2025 baada ya kuzidiwa maarifa na wenyeji Cameroon 4-1 katika mechi ya Kundi J mjini Yaounde, Ijumaa, Oktoba 11, 2024.
Dakika 45 za kwanza zilitamatika wenyeji Cameroon (nambari 53 duniani) wakiwa juu 3-1 baada ya kuona lango kupitia kwa nahodha Vincent Aboubakar (penalti dakika ya nane), Martin Hongla (39) na mshambulizi wa Brentford, Bryan Mbeumo kutokana na asisti ya Christian Bassogog (43).
Mvamizi wa Al Duhail, Michael Olunga, alifungia wenyeji wa AFCON2027 Kenya (nambari 102 duniani) bao dakika ya 41 baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Eric “Marcelo” Ouma anayechezea Rakow Czestochowa nchini Poland.
Kenya ilitarajiwa kuvamia ngome ya Cameroon kutafuta magoli zaidi, lakini ni wenyeji waliozidisha mashambulizi na kuonana vyema, huku Bassogog akiimarisha uongozi wa Indomitable Lions hadi 4-1 dakika ya 55 baada ya Kenya kufanya kosa katika safu ya ulinzi.
Martin Ndzie kisha alichezea nambari Anthony Akumu vibaya nje ya kisanduku na kuipa Kenya nafasi nzuri ya kupata bao la pili dakika ya 73, lakini Onana alikuwa macho na kupangua frikiki hiyo.
Kocha Engin Firat alianzisha Patrick Matasi, Eric Ouma, Sylvester Owino, Daniel Anyembe, Amos Nondi, Anthony Okumu, Richard Odada, Timothy Ouma, Duke Abuya, Olunga na Ronney Onyango. Olunga alikuwa akirejea ulingoni baada ya kuwa shabiki mwezi Septemba wakati Kenya ilitoka 0-0 dhidi ya Zimbabwe na kuchapa Namibia 2-1.
Cameroon nao walianzisha Andre Onana, Christopher Wooh, Michael Ngadeu, Tolo Nouhou, Jackson Tchatchoua, Carlos Baleba, Zambo Anguissa, Hongla, Bassogog, Mbeumo na Aboubakar.
Mara ya mwisho Kenya na Cameroon walikuwa wamekutana katika mechi za kufuzu kushiriki Afcon ilikuwa mwaka 1997 wakati walitoka 0-0 mjini Nairobi (Februari 23, 1997) na 1-1 mjini Yaounde (Julai 27, 1997).
Baada ya michuano mitatu ya kwanza, Cameroon wanaongoza Kundi J kwa alama saba wakifuatiwa na Zimbabwe (tano), Kenya (nne) na Namibia (sifuri).
Kenya wataalika Cameroon katika mechi ya marudiano hapo Oktoba 14 mjini Kampala, Uganda kwa sababu kwa sasasa hawana uga unaotimiza viwango vya kimataifa vya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) wala duniani (FIFA). Nyuga za Kasarani na Nyayo zimefungwa kufanyiwa ukarabati.