Ishara Guardiola ataungana upya na Messi Barcelona 2021
CHRIS ADUNGO Na MASHIRIKA
MFANYABIASHARA Victor Font ambaye anapigiwa upatu kuwa Rais mpya wa Barcelona, amesema kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kumrejesha kocha Pep Guardiola uwanjani Nou Camp.
Guardiola aliondoka Barcelona akiwa kocha mnamo 2012 na kwa sasa anawanoa Manchester City. Mkataba wake ugani Etihad unatarajiwa kutamatika mwishoni mwa msimu ujao wa 2021.
Akiwa Barcelona, Mhispania huyo ambaye pia aliwahi kuchezea Barcelona aliwaongoza miamba hao kusajili ushindi katika mechi 179 kutokana na 247. Alinyanyua jumla ya mataji 14 yakiwemo matatu ya La Liga na mawili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Aidha, amesisitiza kuwa kibarua chake kingine cha kwanza akishika hatamu za uongozi kambini mwa miamba hao wa soka ya Uhispania ni kumsadikisha nyota Lionel Messi astaafu akivalia jezi za kikosi hicho.
Font yuko pazuri zaidi kuwa mrithi wa Josep Maria Bartomeu aliyejiuzulu kambini mwa Barcelona mnamo Oktoba 17, 2020 wiki chache kabla ya mashabiki wa kikosi hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Kujiuzulu kwa Bartomeu kunajiri miezi saba baada ya usimamizi wa Barcelona kushtumiwa kwa usimamizi mbaya wa fedha na kudorora kwa matokeo ya kikosi hicho kilichopokezwa kichapo cha 8-2 na Bayern Munich kwenye robo-fainali za UEFA msimu uliopita wa 2019-20.
Font ambaye alikuwa mshindani wa pekee aliyetarajiwa kumenyana na Bartomeu katika uchaguzi ujao wa urais wa Barcelona sasa huenda akachaguliwa bila kupingwa.
“Klabu inahitaji kusukwa upya na mfumo mzima wa uongozi kuondolewa. Sisemi hivi kwa niaba ya kocha au wachezaji. Hizi ni fikira na hisia zangu binafsi. Wakati umefika kwa usimamizi wa Barcelona kufikiria sana na kusikia kilio cha wazalendo kindakindaki wa kikosi hiki na kutilia maanani maoni ya watu wengine ambao wameokana duni machoni pa wengine,” akasema Font katika mawazo yaliyotiliwa mkazo na beki Gerard Pique.
“Nitakuwa wa kwanza kuagana rasmi na Barcelona iwapo hawatawazia kusajili wanasoka wapya na kuisuka upya kabisa benchi ya kiufundi baada ya kujizulu kwa Bartomeu,” akatanguliza nyota huyo wa zamani wa Manchester United.
“Tuliwahi kuonekana kufika mwisho wa safari na dalili zote kuashiria kwamba tumesambaratika. Haijakuwa mara ya kwanza, ya pili au ya tatu. Hatujakuwa katika mkondo mzuri na hali iliyotukabili mwishoni mwa msimu uliopita ilikuwa ya kutisha na kusikitisha zaidi,” akasema Pique.
“Makocha na wachezaji hupishana katika kila kikosi. Lakini miaka mingi imepita tangu ushawishi wa Barcelona uhisike katika ulingo wa soka ya bara Ulaya.”
“Lazima tujisake upya ndani kwa ndani na kuamua nini kitakachokuwa bora kwa klabu ndipo tujikomboe. Matokeo mabaya ya Barcelona hadi kufikia mwisho wa msimu jana hayastahimiliki, hayakubaliki kabisa, yalitia aibu na yalitudunisha.”
“Ilikuwa vigumu sana kujihusisha na matokeo hayo kwa wakati fulani, ila nina matumaini kwamba yatakuwa kiini cha mwanzo mpya. Mwanzo wa mabadiliko muhimu ambayo yanahitaji kufanyika haraka iwezekanavyo chini ya uongozi mpya,” akasisitiza Pique kwa kutaka Barcelona kubadilisha jina la uwanja wa Camp Nou na kuuita Lionel Messi Stadium.
Nusura Barcelona wapoteze huduma za Messi mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 baada ya nahodha huyo kuwasilisha ombi la kutaka aachiliwe kuondoka uwanjani Camp Nou.
Ombi la Messi liliamsha kiu ya baadhi ya vikosi maarufu vya bara Ulaya kutaka kumsajili japo akaishia kuwa kivutio kikubwa zaidi kambini mwa Manchester City nchini Uingereza.
Hata hivyo, Messi alipiga abautani ya dakika za mwisho na kufutilia mbali mipango yake ya kuhama kwa hofu ya kuvuruga zaidi uhusiano wake na Barcelona waliomlea na kumkuza kitaaluma.
Font na Pique pia wamewataka Barcelona kuazimia haja ya kuwaajiri baadhi ya wanasoka wao wa zamani wakiwemo Xavi Hernandez, Andreas Iniesta na Carles Puyol.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi kambini mwa Barcelona, mnamo Julai 2020 baada ya wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi ya kujiuzulu.
Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliong’atuka ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.
Katika barua yao ya kujiuzulu, sita hao waliangazia pia jinsi Barcelona inavyokosa mpango madhubuti wa kukabiliana na athari za kifedha zitakazotokana na virusi vya homa kali ya corona.
Katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji, Barcelona waliagana na idadi kubwa ya wanasoka wakiwemo Arthur Melo aliyetua Juventus, Ivan Rakitic aliyejiunga na Sevilla na Nelson Semedo aliyeyoyomea Wolves.
Wengine ni Arturo Vidal aliyesajiliwa na Inter Milan na Luis Suarez aliyeingia katika sajili rasmi ya Atletico Madrid.
Mnamo Septemba, kampeni ya kupigwa kwa kura ya kutokuwa na imani na Bartomeu zilipata uungwaji mkono miongoni mwa wadau wa kikosi cha Barcelona.
Bartomeu alichaguliwa kuwa Rais wa Barcelona mnamo 2014 na uongozi wake umekashifiwa pakubwa kiasi cha kuhusishwa na maamuzi ya Messi kutaka kuondoka ugani Camp Nou.
Mpango wa kuondolewa kwa Bartomeu kupitia kura ya maoni ulifichuliwa na vinara wa Barcelona siku moja baada ya Messi kuwasilisha barua ya kutaka kuachiliwa kuondoka Camp Nou.
Kufikia sasa, saini 20,731 kutoka kwa mashabiki na wasimamizi wa Barcelona wanaounga mkono mpango huo zimepatikana, kumaanisha kwamba Bartomeu angeondolewa mamlakani kupitia kura ya wadau kutokuwa na imani naye hata kama asingejiuzulu.
Ili kufanikisha maandalizi ya kura hiyo, jumla ya saini 16,500 pekee ndizo zilizohitajika kuwasilishwa na kukaguliwa na wahusika kabla ya Bartomeu, 57, kuondolewa kupitia refarenda chini ya kipindi cha miwili mitatu ijayo. Bartomeu alitarajiwa kukamilisha rasmi kipindi chake cha uongozi cha mihula miwili mnamo Machi 2021.
Iwapo kura ya kutokuwa na imani naye itaandaliwa, basi atakuwa rais wa tatu wa Barcelona kuondolewa mamlakani kwa jaribio la njia hiyo baada ya Josep Lluis Nunez mnamo 1998 na Joan Laporta mnamo 2008. Mpango wa kung’atuliwa kwa wawili hao kupitia refarenda miaka hiyo haukufaulu.