Kane anusia kumaliza laana ya kutoshinda taji Bayern ikipiga Leverkusen
MSHAMBULIZI Harry Kane anakaribia kumaliza nuksi ya kutoshinda taji na timu yoyote amechezea ya watu wazima.
Mvamizi huyo ataendelea kujiweka pazuri iwapo viongozi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich, watalima mabingwa watetezi Bayer Leverkusen wanaokamata nafasi ya pili, leo usiku.
Kane hakushinda chochote kambini mwa Tottenham Hotspur baada ya kuichezea jumla ya mechi 317 kutoka msimu 2011-2012 hadi 2022-2023.
Alihama Spurs baada ya kuifungia mabao 213 na kuchangia asisti 47. Aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu 2015-2016 kwa kuchana nyavu mara 25, msimu 2016-2017 (mabao 29) na 2020-2021 (23), lakini taji la timu likamponyoka.
Alijiunga na Bayern msimu 2023-2024 na kuibuka mfungaji bora akiwa na mabao 36 kwenye Bundesliga ambayo miamba hao walimaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya washindi Leverkusen na nambari mbili Stuttgart.

Mambo hayajakuwa tofauti katika timu ya taifa ya Uingereza ambapo amesakata mechi 103 na kuifungia magoli 69 tangu aitwe kikosini na kocha Roy Hodgson mwezi Machi 2015.
Hajashinda taji na Three Lions ya Uingereza isipokuwa tuzo ya kibinafsi ya mfungaji bora kwenye Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi na Kombe la Euro 2024 mjini Berlin.
Iwapo Bayern itachabanga Leverkusen katika mechi ya raundi ya 22 leo, basi vijana wa kocha Vincent Kompany watafungua mwanya wa alama 11 dhidi ya vijana wa kocha Xabi Alonso ambao ni wapinzani wa karibu.
Kane anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Bundesliga baada ya kucheka na nyavu mara 21, mabao saba dhidi ya mpinzani wa karibu Patrik Schick wa Leverkusen.
Bayern hawakushinda chochote katika msimu wa kwanza wa Kane 2023-2024. Ni mara ya kwanza Bayern mikono mitupu katika kipindi cha miaka 12.