Michezo

KCB na Mara Sugar zawika, Shabana na AFC kivangaito

Na CECIL ODONGO NA WYCLIFFE NYABER February 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CECIL ODONGO NA WYCLIFFE NYABERI

KOCHA wa KCB Patrick Odhiambo jana alisema kuwa wanalenga kujenga matokeo mazuri baada ya kumaliza ukame wa kutopata ushindi kwa kuibwaga Murangá Seal 2-0 kwenye Ligi Kuu (KPL).

Mchuano huo uligaragazwa katika uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.
Odhiambo jana alisema lilikuwa jambo la kusikitisha kuwa waliongoza jedwali la KPL kwa kipindi kirefu ila wakaporomoka na kupitwa na wapinzani.
“Tumekuwa na wimbi la matokeo mabaya na nilikuwa na mazungumzo na wachezaji wangu jinsi ambavyo tungeweza kujiinua na kushinda mechi zetu. Kucheza pamoja, kuelewana na kufuata maagizo ya kocha ndiyo yatatusaidia kutumia matokeo haya kuwika kwene mechi zijazo,’ akasema Odhiambo.
Katika mechi tisa zilizopita, KCB ilikuwa imepata ushindi mara moja pekee ikipata ushindi wa 3-2 dhidi ya Mara Sugar katika uga wa Awendo, Kaunti ya Migori.
“Ligi tayari imefikia katikati na lazima tujizatiti kupunguza mwanya wa alama kati yetu na wapinzani wetu. Hii ndiyo maana lazima tuendeleze wimbi la ushindi kwa sababu hata nasi tunataka ushindi,” akasema Odhiambo.
Jana wanabenki hao walipata mabao yao mawili kupitia mshambuliaji Vincent Ondabu.
Katika mechi nyingine Mara Sugar nayo ilitoka nyuma na kuadhibu FC Talanta 4-1 katika uga wa Awendo, Kaunti ya Migori.
Talanta walikuwa wa kwanza kuliona lango la wapinzani wao kunako dakika ya 37 kupitia kwa mchezaji Alex Kipruto, aliyefyatya shuti kali lililomwacha Melinda lango wa Mara Sugar FC Felix Adoyo hoi.
Kipindi cha pili kilipoanza, wenyeji Mara Sugar FC tena, walizidisha mashambulizi na juhudi zao zilizaa matunda dakika tatu baadaye wakati Robert Obaga aliwafungia bao la kusawazisha.
Kunako dakika ya 50, Mara Sugar FC walipata bao lililowaweka kifua mbele kupitia mchezaji Erick Juma. Bao hilo liliwawezesha wanasukari hao kuudhibiti mchezo kikamilifu.
Kukiwa kumesalia dakika 10 mchezo kukamilika, vijana wa kocha Benedict Wanjala walijizolea mabao mengine mawili kutoka kwa Joseph Okwenda katika dakika za 82 na 89.
Mibabe AFC Leopards walitoka sare tasa dhidi ya Kariobangi Sharks ugani Dandora huku Posta Rangers ikiadhibu Shabana 2-1 uga wa Kenyatta.
Mabao ya Posta Rangers yalifungwa na Shami Kibwana na Curtis Wekesa huku Dennis Okoth akifungia Shabana.
Ulinzi Stars pia waliagana sare tasa dhidi ya Kakamega Homeboyz uwanjani Dandora