KPL kuamua hatima ya ligi wiki hii
Na CECIL ODONGO
USIMAMIZI wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) utaandaa mkutano wiki hii kuamua hatima ya msimu huu baada ya serikali kuongeza muda wa kafyu kwa siku 21 zaidi kutokana na janga la Covid-19.
Rais Uhuru Kenyatta mnamo Jumamosi alitangaza kwamba kafyu hiyo sasa itatamatika Juni 6, 2020, wakati ambapo serikali itatoa taarifa tena kama itaongezwa au la.
Afisa Mkuu wa KPL Jack Oguda ameeleza kwamba mkutano huo wa kamati kuu ya KPL utaandaliwa siku ambayo ataitangaza ambapo kauli ya mwisho kuhusu hatima ya msimu itatolewa.
Msimu huu mwanzoni uliratibishwa kwamba ungetamatika Mei 24, 2020.
“Tutakuwa na mkutano wiki hii na tutawajuza siku. KPL ndiyo ilisitisha mechi za ligi kutokana na amri ya serikali kuhusu mikusanyiko ya watu maeneo ya umma na tutawaeleza hatima ya msimu huu baada ya siku za kafyu kuongezwa tena,” akasema Oguda.
Mnamo Aprili 30, 2020, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa alitawaza Gor Mahia kama mabingwa wa KPL na pia kuteremsha ngazi Chemelil Sugar na SoNy Sugar.
Hata hivyo, Chemelil wakiongozwa na mmiliki wao Moses Adagala pamoja na usimamizi wa KPL uliwasilisha kesi ya kuupinga uamuzi wa FKF mbele ya Korti ya Kutatua Mizozo ya Michezo (SDT).
Mwenyekiti wa SDT John Ohaga alibatilisha uamuzi wa FKF na kutangaza kwamba ataanza kesi hiyo mnamo Mei 26.
Hata hivyo, Oguda alisema kwamba uamuzi wa Jaji Ohaga hauwazui kutangaza msimamo wao kuhusu hatima ya msimu huu.
Kabla ya KPL kusitishwa kwa muda usiojulikana mnamo Machi, K’Ogalo walikuwa wakiongoza msimamo wa jedwali kwa alama 54, saba mbele ya nambari mbili Kakamega Homeboyz, zikiwa zimesalia mechi 10 msimu utamatike.
Kutawazwa kwa Gor kulipingwa na baadhi ya timu, huku klabu kadhaa zikipigia upato kufutiliwa mbali kwa msimu huu.