Kuchezea Gor Mahia kuliniandaa kwa soka ya ushindani mkubwa – Musa Mohammed
Na CHRIS ADUNGO
NAHODHA wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed, amekiri kwamba kuchezea mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kulimwandaa vyema zaidi kwa soka anayoitandaza kwa sasa kambini mwa Nkana Red Devils nchini Zambia.
Musa alivalia jezi za Gor Mahia kwa kipindi cha miaka 10, tisa kati ya miaka hiyo akiwa nahodha.
“Gor Mahia ni klabu kubwa inayojivunia mashabiki wengi ambao siku zote hukupa presha ya kukusukuma kuwa bora. Yeyote ambaye amewahi kuchezea Gor Mahia basi ana uwezo wa kutamba katika ligi yoyote barani Afrika,” akasema Musa anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuhamia Yangas SC nchini Tanzania muhula ujao.
Hata hivyo, sogora huyo matata wa Harambee Stars ameeleza ukubwa wa tofauti katika usimamizi wa Nkana na Gor Mahia.
“Ni afueni tele kuchezea hapa Zambia. Maafisa wa klabu wanawastahi sana wachezaji na wanasoka hutekelezewa yote kwa mujibu wa makubaliano kwenye kandarasi zao. Kwa kifupi, kila kitu huendeshwa kwa utaalamu zaidi kambini mwa Nkana ikilinganishwa na Gor Mahia,” akasema.
Kwa mujibu wa Musa, kuzoea maisha nchini Zambia hakukumtatiza pakubwa hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya wanasoka wanasakatia vikosi kadhaa vya Ligi Kuu ya Zambia (ZSL).
“Ilikuwa rahisi kuzoea mazingira hayo mapya kwa kuwa nilikuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara na baadhi ya masogora wa Kenya wanaochezea Zambia. Walinishauri vilivyo na nilikuwa nafahamu ya kutarajia hata kabla ya kutua Nkana FC,” akaongeza.
Musa alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri. Anasema aliridhishwa pakubwa na maandalizi ya kikosi hicho nchini Ufaransa na bonasi ambazo kwa sasa wamezipokea kutokana na ushindi wao dhidi ya Tanzania ni hamasa tele kwa wanasoka wengi kutaka sasa kuiwajibikia timu ya taifa.
“Bonasi kutoka kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ni motisha kubwa japo hamasa zaidi katika baadhi ya vibarua vya Harambee Stars ni fursa ya kuvaana na wanasoka wa haiba kubwa katika ulingo wa soka ya kimataifa. Ilikuwa tija na fahari tele kukabiliana na Sadio Mane wa Senegal na Riyad Mahrez wa Algeria katika fainali zilizopita za AFCON.”
Katika juhudi za kumzuia Musa kuyoyomea Yanga, Nkana wapo radhi kuongeza mshahara wake maradufu hadi ufikie Sh5 milioni kwa mwezi. Nyota huyo amekuwa akiviziwa pakubwa na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Zamalek SC (Misri), St George (Ethiopia) na Kabwe Warriors (Zambia).
Musa aliingia katika sajili rasmi ya Nkana mnamo Julai 2018 baada ya kuagana na FK Tirana ya Albania ambayo pia imewahi kujivunia huduma za Wakenya Francis Kahata, Eric ‘Marcelo’ Ouma na Kenneth Muguna.
Chini ya unahodha wake, Harambee Stars waliambulia nafasi ya pili katika kipute cha kuwania ubingwa wa Hero International Cup nchini India mnamo 2018. Awali, alikuwa amewaongoza Stars kunyakua ubingwa wa Cecafa Senior Challenge Cup 2017 baada ya kuwazidi maarifa Zanzibar Heroes kwa mikwaju ya penalti uwanjani Kenyatta, Machakos.
Hadi kufikia sasa, klabu za Zambia zinawapa hifadhi Wakenya David ‘Calabar’ Owino, Jesse Jackson Were (wote wa Zesco United); John Mark Makwatta (Buildcon FC); Ian Otieno, Andrew Tololwa (Red Arrows), Ismail Dunga, Shaban Odhoji (wote wa Napsa Stars), Harun Shakava, Duncan Odhiambo, Duke Abuya na Musa (wote wa Nkana FC).