Michezo

Mary Njoroge ateuliwa kusimamia mechi za Kombe la Dunia U-20

May 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Mary Njoroge yuko katika orodha ya maafisa sita kutoka Bara Afrika walioteuliwa kusimamia mechi katika Kombe la Dunia la Wanawake wasiozidi umri wa miaka 20 nchini Ufaransa hapo Agosti 5-24, 2018.

Katika orodha hiyo iliyotangazwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Aprili 9, Njoroge pamoja na Lidwine Rakotozafinoro (Madagascar) na Victoire Queency (Mauritius) watakuwa marefa wasaidizi (wanyanyuaji vibendera).

Njoroge pamoja na Wakenya wenzake, refa Agneta Itubo na refa msaidizi Jane Cherono walisimamia mechi ya marudiano ya kufuzu kushiriki kombe hili kati ya Djibouti na Burundi mnamo Agosti 5, 2017 ambayo wageni Burundi walishinda 2-1 katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza.

Kenya haikuwa na afisa yeyote wa kusimamia mechi katika makala ya mwaka 2012, 2014 na 2016.

Muethiopia Lidya Tafesse Abebe na raia wa Malawi Gladys Lengwe ni marefa pekee kutoka Afrika watakaopuliza kipenga nchini Ufaransa. Timu za taifa za Nigeria na Ghana zilifuzu kuwakilisha Bara Afrika katika mashindano haya ya nchi 16.

Ghana, ambayo ilizima kampeni ya Kenya ya kufika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kwa kuiliza 5-0 mjini Cape Coast na 5-1 mjini Machakos katika raundi ya pili, iko katika Kundi A pamoja na Ufaransa (wenyeji), New Zealand na Uholanzi. Mabingwa mara mbili wa Afrika Nigeria watalimana na Haiti, washindi wa medali ya fedha mwaka 2004 na 2006 Uchina na mabingwa mara tatu Ujerumani katika Kundi D.

Timu ya Nigeria inasalia timu iliyofanya vyema katika kombe hili kutoka Afrika ilipomaliza katika nafasi ya pili mwaka 2010 na 2014 na nambari nne mwaka 2012. Marefa 15 na wanyanyuaji vibendera 30 watakuwa nchini Ufaransa kwa makala haya ya tisa.