Michezo

McCarthy imani tele Harambee Stars itafuzu Kombe la Dunia

Na CECIL ODONGO March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa Harambee Stars Benni McCarthy anaamini kikosi chake bado kina nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kupambana vikali na kutoka sare ya 3-3 dhidi ya Gambia mnamo Alhamisi usiku kule Cote d’Ivoire.

Stars Jumapili hii itakuwa na kibarua kingine, ikivaana na Gabon katika uga wa kitaifa wa Nyayo. Itakuwa mara ya kwanza ambapo Kenya itakuwa ikicheza nyumbani baada ya kuwajibikia mechi za awali za kufuzu Kombe la Afrika nje ya nchi.

Kenya haikuwa na uga kwa sababu nyuga zake zilikuwa zikiendelea kukarabatiwa kwa ajili ya mechi ya Mashindano ya Soka ya wanasoka wanaoshiriki ligi za nyumbani, CHAN na Kombe la Afrika 2027 (AFCON).

Kuelekea mechi ya Gabon, Kenya ipo katika Kundi F kwa alama sita baada ya mechi tano huku Gambia ikiwa nambari tano kwa alama nne. Gabon ina alama 12 huku Ushelisheli ikiwa haina alama zozote.

Burundi ambayo inatarajiwa kucheza na Cote d’Ivoire Ijumaa usiku ina alama saba kisha mabingwa hao watetezi wa AFCON wana alama 10.

“Hatuwezi kukataa tamaa kwa sababu bado tunaamini wapinzani wetu watadondosha alama. Gambia inaweza kupiga Cote d’Ivoire na Gabon na Kenya pia inaweza kupata ushindi dhidi ya nchi hizo zilizochukua uongozi wa mapema,”  akasema McCarthy.

“Kuna mechi tano zilizosalia na alama 15 ambazo zinapiganiwa kwa hivyo tuna imani  kuwa tutapambana na kufuzu,” akaongeza McCarthy.

Ni timu ya kwanza kwenye kundi F itafuzu moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia 2026 ambalo litaandaliwa Canada, Amerika na Mexico. Kuna makundi mengine manane ambako washindi pia watafuzu kipute hicho moja kwa moja.

Hata hivyo, timu nne bora zitakazomaliza nafasi ya pili kwenye makundi hayo nazo zitashiriki mchujo ambapo mshindi atashiriki mchujo mwingine wa Fifa ambako mshindi atatwaa tikiti ya kucheza Kombe la Dunia.

Kwenye mechi ya Jumapili, Kenya itakuwa na mlima wa kukwea kwa kuwa Gabon si mpinzani rahisi. Kenya ipo nafasi ya 125 katika orodha ya viwango vya Fifa huku Gabon ikiwa nambari 84.

Kikosi cha Gabon chini ya Kocha Thierry Mouyouma kiliwasili Nairobi Ijumaa na kina nyota Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye ni mfungaji bora wa timu ya taifa kisha pia yupo kiungo Denis Bouanga.

“Gabon ni mpinzani mgumu na nawaomba mashabiki wajaze uwanja wa Nyayo ili kuwapa vijana wetu motisha dhidi yao ndipo tupate ushindi nyumbani,” akasema McCarthy.

Mashabiki ambao watashuhudia mechi hiyo watalipia Sh10,000 kuketi kwenye eneo la wageni mashuhuri zaidi, kisha wale wa eneo la wageni mashuhuri, Sh1,000.

Wale watakaoketi eneo la kawaida watalipa Sh300 kisha pia Sh300 zitalipwa na wale watakaokuja na magari yao na kuyaegesha Nyayo.