Mourinho naye pia ajumuishwa katika wanaoweza kuwa kocha mkuu wa Brazil
JOSE Mourinho anaaminika kuwa katika orodha ya makocha wa timu ya taifa ya Brazil ambaye inaangalia kujaza nafasi ya kocha mkuu baada ya Dorival Junior kutimuliwa mnamo Machi 28, 2025.
Kocha huyo Mreno, ambaye kwa sasa anatia makali Fenerbahce, yuko katika orodha inayojumuisha pia Mwitaliano Carlo Ancelotti (Real Madrid), Mhispania Pep Guardiola (Manchester City), Wareno Jorge Jesus (Al Hilal, Saudi Arabia) na Abel Ferreira (Palmeiras, Brazil) na Mbrazil-Mwitaliano Renato Gaucho (Fluminense).
Gaucho alijiunga na Fluminense Aprili 3, 2025 kama kocha wake kwa mara ya sita.
Ancelotti, 65, amefanya majukumu ya kocha tangu Julai 1992 ikiwemo katika klabu za Juventus, AC Milan, Chelsea, PSG na Bayern Munich. Kandarasi yake na Madrid itakatika Juni 2026.
Guardiola, 54, amekuwa kocha tangu Julai 1, 2007 na ameongoza Barcelona, Bayern na City. Kandarasi yake na City inatarajiwa kukatika Juni 2027.
Mourinho, 62, amefanya kazi ya ukocha tangu Julai 1, 1987. Miongoni mwa klabu ambazo amenoa ni Sporting CP, FC Porto, Barcelona, Real Madrid, Chelsea, Manchester United, Tottenham na AS Roma. Kandarasi yake na Fenerbahce inafaa kutamatika Juni 2026.
Jesus, 70, anafaa kuondoka Al Hilal mwezi Juni 2025. Abel Ferreira, 46, yuko Palmeiras hadi Desemba 2025, naye Gaucho, 62, ametwikwa majukumu ya kuongoza Fluminense hadi Desemba 2025.
Kampuni nyingi za kubeti zinapigia upatu mkubwa Jesus kuchukua usukani kuongoza mabingwa mara tano wa dunia, Brazil.