Msiidhalilishe Man City, Klopp aonya
Na CHRIS ADUNGO
KIPIGO cha 3-0 kwenye robo fainali za Klabu Bingwa Ulaya kilitangulia kingine cha 3-2 kwenye debi ya Manchester baada ya kuongoza katika kipindi cha kwanza kwa goli mbili mtungi.
Hata hivyo, licha ya Liverpool kupigiwa upatu kuingia nusu failnali baada ya mechi ya marudiano ugani Etihad Jumanne usiku, kocha Jurgen Klopp hajabadilisha mtazamo wake kuhusu timuwatakayochuana nayo.
Alipoulizwa iwapo Man City walikuwa wepesi wa kuachilia mabao kuingia kwa lango lao, Mjerumani huyo alisema: “La hasha, sidhani kitu kama hicho.
“Wamekuwa na msimu bora zaidi lakini wao ni binadamu, shukuru Mola. Wamekuwa na matokeo mawili ambayo labda hakuna aliyetarajia.
“Man United walikuwa na bahati, katika kipindi cha kwanza, Man City wangefunga mabao sita na Man United hawakuwa na mechi ya katikati ya wiki, nayo City ilifanya mageuzi ya kikosi.
“Walipotupiga 5-0 mwanzoni mwa msimu, kila mtu alijionea makali ya City hata kama tulikuwa na kadi nyekundu. Wana kocha bora zaidi ulimwenguni.
“Ni kweli ni wazuri lakini hakuna mechi bila kufanya makosa duniani. Mchezo huu haukuruhusu kuwa bora kiasi cha kutofanya makosa.”
“Sidhani Barcelona wanafikiri kuwa washafika nusu fainali baada ya kupiga Roma 4-1, kwa kuwa hii ni soka na una nafasi ya kujinyayua na kupata ushindi.
“Man City wana nafasi ya kuingia nusu fainali. Watu wengi wanafikiri Liverpool inafuzu lakini wanaweza kupoteza. Pia tuna nafasi ya kushinda,” amesema kocha huyo.