Nairobi City Stars yangurumia Gor na kudidimiza matumaini yao ya kutwaa KPL
GOR MAHIA Alhamisi ilipata pigo kwenye juhudi zake za kutetea taji la Ligi Kuu (KPL) baada ya kutandikwa 2-1 na Nairobi City Stars waliokuwa wakivuta mkia kwenye uga wa Dandora Nairobi.
Kwenye mechi nyingine iliyogaragazwa Alhamisi uwanja wa Dandora, Kariobangi Sharks ilishinda KCB 1-0 na kuendelea na juhudi za kukwepa shoka la kutimuliwa KPL.
Ugani Dandora, makosa ya kipa Gad Mathews yalitunuku City Stars bao la kwanza ambalo lilifungwa na Hansel Ochieng’ mapema kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, Benson Omala alisawazishia Gor dakika chache baadaye na kuwapa mashabiki wa Gor matumaini kwamba timu yao ingerejea mchezoni.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Vincent Owino aliwafungia Simba wa Nairobi, bao ambalo lilitokana na masihara langoni mwa Gor.
City Stars pia ilishinda Gor 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Oktoba 28 mwaka uliopita.
Kushindwa huko kuliwaghadhabisha mashabiki wa Gor ambao waliwazomea wachezaji na benchi ya kiufundi kwa sababu walikosa kupunguza mwanya kati yao na viongozi Kenya Police na nambari mbili Tusker. Baadhi hata walihusu kichapo hicho na kuvamiwa kwa hekalu la Freemason Jumatano, uvamizi uliotekelezwa na Kaunti ya Nairobi kutokana na deni la Sh19 milioni, ada ya ardhi.
Kenya Police ilipigwa 2-1 na Kakamega Homeboyz mnamo Jumatano uga wa Mumias Sports Complex huku Tusker ikipigwa 2-0 na FC Talanta.
Kushindwa huko kuliacha Gor kwenye nafasi ya tatu kwa alama 53 baada ya mechi 30. Kenya Police (alama 58), Tusker (alama 55) zimecheza mechi 31 na zimebaki na mitanange mitatu tu msimu huu utamatike.
Shabana ina alama 52 huku Kakamega Homeboyz ikiwa na alama 51 pia zikiwa zimesalia na mechi tatu msimu huu utamatike.
Timu hizo zote bado zina nafasi ya kuwahi ubingwa wa KPL msimu huu.
“Haya ni matokeo yanayoghadhabisha mno kwa sababu yanapiga breki juhudi zetu na kupunguza mwanya kati yetu na wapinzani wetu. Hatujacheza vizuri wala hatukujituma sana kuhakikisha tunapata ushindi,” akasema Kocha wa Gor Sinisa Mihic.
Ushindi huo ulitoa City Stars mkiani na sasa wana alama 30 baada ya mechi 31 katika nafasi ya 17 wakiendelea kupambana kubaki KPL.
Bao la Kariobangi Sharks lilifungwa na Humprey Aroko katika dakika ya 66 na kuzidisha masaibu ya KCB. Sharks wako nafasi ya 12 kwa alama 36 baada ya mechi 31 nao KCB wapo nambari saba kwa alama 41.