Michezo

Ona, pesa ambazo Jose Mourinho amezoa kwa kufutwa kazi ni za kukausha bahari!

Na MASHIRIKA November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Jose Mourinho alipotimuliwa na Manchester United mnamo 2018, miezi michache tu baada ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumpa mkataba mpya wa miaka miwili, klabu hiyo ilimlipa Sh4 bilioni.

Pesa hizo zinatosha kujenga zaidi ya kilomita moja na nusu ya Barabara ya Nairobi Express Way na ingemchukua Mkenya anayelipwa ujira wa Sh400,000 kwa mwezi takriban miaka 830 kufikisha kiasi hicho cha fedha!

Alipoagana na AS Roma mwanzoni mwa mwaka huu, miezi sita kabla ya mkataba wake kutamatika rasmi, Mreno huyo alilipwa fidia ya Sh609 milioni. Hiyo ilikuwa mara ya sita kwa Mourinho kutimuliwa baada ya kupigwa kalamu na Chelsea (mara mbili), Real Madrid, Man-United na Tottenham Hotspur.

SOMA PIA: Hivi huyu Amorim ndio atakuwa Mourinho mpya pale Man Utd?

Mourinho, 60, ni miongoni mwa wakufunzi wanaosakwa sana duniani na hulipwa mshahara mnono popote anapokwenda. Ina maana kuwa fidia yake pia huwa kubwa kila anapofutwa kazi.

Kufikia sasa, kocha huyo anayenoa kikosi cha Fenerbahce nchini Uturuki, anakadiriwa kupata takriban Sh16.2 bilioni kutokana tu na kuachishwa kazi na klabu mbalimbali katika taaluma yake ya ukufunzi.

Chelsea walimlipa Sh5.2 bilioni walipomtimua mara mbili – Sh3.6 bilioni mnamo 2007 kisha Sh1.6 bilioni alipofukuzwa ugani Stamford Bridge kwa mara ya pili mwaka wa 2015. Alikabidhiwa pia kitita cha Sh3.7 bilioni na Real Madrid alipoondoka Santiago Bernabeu mnamo 2013.

Mourinho alikuwa akilipwa mshahara wa Sh3 bilioni kwa mwaka alipojiunga na Tottenham Hotspur mnamo Novemba 2019. Hata hivyo, alihudumu katika kikosi hicho kwa miezi 17 na akalipwa kiasi hicho cha pesa alipofutwa kazi akisalia na miaka miwili kwenye kandarasi yake.

SOMA PIA: Ilikuwa vigumu sana kushinda mechi wakati wa Mourinho – Pogba

Hakuna kocha mwingine aliyewahi kupata faida kubwa ya kifedha kutokana na kufutwa kazi kuliko Mourinho almaarufu ‘The Special One’. Antonio Conte, ambaye pia aliwahi kunoa Chelsea (2016-2018), alilipwa Sh7.5 bilioni Spurs walipomfurusha mnamo Machi 2023.

Kati ya wakufunzi wengine waliowahi kulipwa vinono baada ya kutimuliwa na klabu zao ni Thomas Tuchel (Sh2.2 bilioni akiondoka Chelsea na Sh1.4 bilioni akifutwa na Bayern), Xavi Hernandez (Sh2.1 bilioni akitoka Barcelona) na Ole Gunnar Solskjaer (Sh1.3 bilioni akitimuliwa Man-United).

Marco Silva wa Fulham alitia mfukoni Sh752 milioni alipofurushwa Everton naye Roberto Mancini Sh2.8 bilioni alipoondoka Saudi Arabia. Kocha huyo raia wa Italia alipokezwa Sh1.7 bilioni alipofutwa kazi na Man-City mnamo 2013 na Inter Milan wakamfidia Sh700 milioni walipomtimua 2008.

Hatua ya Man-United ya kumtimua Erik ten Hag majuzi inatarajiwa pia kuachia miamba hao wa zamani mzigo mzito wa kifedha, ripoti zikionyesha kuwa kocha huyo raia wa Uholanzi atawadai Sh2.7 bilioni, kwa mujibu wa masharti ya mkataba wake. Hizo pia si pesa kidogo za kuokota barabarani!

Pesa za Mourinho kila alipotimuliwa:

Chelsea (mara ya 1) – Sh3.6 bilioni

Real Madrid – Sh3.7 bilioni

Chelsea (mara ya 2) – Sh1.6 bilioni

Man-United – Sh4 bilioni

Tottenham – Sh3 bilioni

AS Roma – Sh609 milioni