Michezo

Raha Kampuni ikisafirisha mashabiki kwa mabasi ya umeme kutazama Kombe la UEFA

Na CECIL ODONGO May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MASHABIKI wengi wa soka Jumamosi walijitokeza Duka la Sarit, mtaani Westlands Nairobi kutazama Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) huku timu zitakazoshiriki fainali zikitarajiwa kujulikana Jumanne na Jumatano.

Kenya ni kati ya mataifa matano Afrika ambayo kombe hilo limetua na limekuwa likizingushwa mataifa mbalimbali katika mabara mengine kwa muda wa mwezi moja uliopita.

Vietnam ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kupokea kombe hilo mnamo Aprili 7. Safari za kuzungusha taji hilo katika mataifa mbalimbali zimekuwa zikidhaminiwa na Kampuni ya Heineken.

Ijumaa, nguli wa soka Ujerumani Bastian Schweinsteiger,  alifikisha kombe hilo kwenye ikulu ya Nairobi ambapo alipokelewa na Rais William Ruto na viongozi wengine serikalini.

Kiongozi wa nchi, shabiki sugu wa Arsenal alisema kuwa anaipigia upato The Gunners kubatilisha kushindwa 1-0 na PSG Jumanne iliyopita, timu hizo zikishiriki mechi ya marudio mnamo Jumatano wiki ijayo jijini Paris.

Nusu fainali nyingine itagaragazwa Jumanne ambapo Inter Milan watakuwa wenyeji wa Barcelona ugani San Siro. Timu hizo ziliagana sare ya 3-3 katika mechi ya mkondo wa kwanza ugani Camp Nou.

Jumamosi, mashabiki walifika Westlands kujionea kombe hilo baada ya kusafirishwa kwa mabasi ya umeme kutokana na udhamini wa Kampuni ya uchukuzi ya Little Cabs.

Mabasi hayo yaliwachukua abiria kutoka Kencom, Junction Mall, TRM na Imaara Mall na wakaona kombe hilo ambalo mashabiki wa Arsenal wana kiu sana cha kulishinda.

“Mabasi yaliyotumika kusafirisha mashabiki yanatumia umeme na kupunguza uchafuzi wa hewa kwa kutoa moshi au gesi kwa kiwango cha chini. Kuwa kati ya wanaoshiriki ziara ya Uefa nchini, kunatupa nafasi ya kuungana na mashabiki wa soka ambao wanathamini sana kipute cha Uefa,” akassema Nyawira Maina, Meneja wa Little Cab nchini.

Kando na mabasi, Little Cabs pia huwa na baiskeli zinazotumia umeme ambazo ziliingia sokoni Machi mwaka huu baada ya mchakato wa kuzivumbua kuchukua miaka miwili.