Michezo

Wenger amtunuka sifa chipukizi Kylian Mbappe

May 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema kwamba chipukizi Kylian Mbappe ndiye aliye na uwezo wa kuendeleza mwenge uliowashwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo katika soka ya kizazi cha sasa.

Ronaldo, 35, na Messi, 32, wamekuwa wakitawala ulingo wa kandanda kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na kwa sasa wanaelekea kuondoka jukwaani na kupisha warithi wao.

Kwa mujibu wa Wenger, hakuna sogora mwingine kwa sasa kuliko Mbappe ambaye ana kipaji na uwezo sawa na unaojivuniwa na Messi na Ronaldo ambao kwa sasa wanachezea Barcelona na Juventus mtawalia.

“Katika umri wangu huu, sijawahi kuona mchezaji aliye na kiwango kikubwa cha ubunifu katika hali yoyote kuliko Messi. Hata hivyo, makali ya wachezaji hawa – Ronaldo na Messi ambao wamekuwa wanasoka bora wa muda wote – yanaelekea kupungua,” akatanguliza Wenger.

“Sasa tunawazia kizazi kingine, na sijaona mwanasoka aliye na uwezo wa Mbappe. Neymar Jr angekuwa mrithi wa moja kwa moja wa Messi na Ronaldo lakini ilivyo kwa sasa, Mbappe anampiku na sote tunajua hivyo,” akasema Wenger.

Mbali na Mbappe ambaye ni mzawa wa Ufaransa, Wenger anahisi kwamba mchezaji mwingine ambaye ana mustakabili angavu katika juhudi za kufukuzana na Mbappe ni chipukizi wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho ambaye kwa sasa anamezewa mate na Liverpool na Man-United.

Wenger amefichua pia kwamba aliwahi kuwa pua na mdomo kuwasajili Ronaldo, Messi na Mbappe katika kipindi chake cha miaka 22 cha ukufunzi kambini mwa Arsenal.

Akiwa na umri wa miaka 18, Ronaldo aliwahi kushiriki mazoezi katika uwanja wa London Colney unaomilikiwa na Arsenal. Licha ya Arsenal kuweka mezani kima cha Sh560 milioni kwa minajili ya huduma za Mreno huyo, kusajiliwa kwake kuligonga ukuta na akahiari kutua Old Trafford kuvalia jezi za Man-United.

Nusura Messi abanduke Barcelona mnamo 2002-03 na kutua Arsenal baada ya Wenger kumshawishi nyota huyo mzawa wa Argentina kubanduka ugani Nou Camp kwa kima cha Sh3 bilioni.

Mbappe, 21, ni sogora mwingine ambaye Wenger alikuwa karibu sana kumsajili mnamo 2016. Licha ya Arsenal kukubali kuweka mezani kima cha Sh300 milioni ili kumshawishi Mbappe kubanduka AS Monaco, fowadi huyo aliteua kuelekea Paris Saint-Germain (PSG).

Badhi ya nyota wengine ambao waliwahi kushawishiwa na Wenger kuingia katika sajili rasmi ya Arsenal na uhamisho wao kutibuka dakika za mwisho ni Virgil van Dijk (Liverpool), N’Golo Kante (Chelsea), Luis Suarez (Barcelona), Raheem Sterling (Man-City), Gareth Bale (Real), Paul Pogba (Man-United), Jamie Vardy (Leicester), Zlatan Ibrahimovic (AC Milan), Gerrard Pique (Barcelona) na Gianluigi Buffon (Juventus).