Habari za Kitaifa

Millie, Amisi na Junet wavuna Otiende akila hu ODM ikitangaza mabadiliko bungeni

Na CECIL ODONGO August 1st, 2024 2 min read

CHAMA cha ODM Jumatano kilitekeleza mabadiliko kwenye uongozi wake bungeni huko Kinara wake Raila Odinga akiwatunuku wandani wake kutoka Nyanza na Magharibi nyadhifa muhimu katika Bunge la Kitaifa.

Kufuatia kuteuliwa Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi kama waziri mteule wa Kawi, nafasi yake bungeni jana ilipewa mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye alikuwa kati ya wasimamizi wa kampeni za Bw Odinga mnamo 2022.

Kabla ya uteuzi huo, Bw Mohamed alikuwa akihudumu kama kiranja wa wachache.

Mabadiliko hayo yalitangazwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Chama  (NEC) ulioandaliwa jijini Nairobi. Nafasi ya Bw Mohamed nayo ilitunukuwa mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.

Katika kamati za bunge, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi atakuwa mwenyekiti mpya wa kamati ya hadhi ya Uhasibu Bungeni. Bw Amisi amemrithi mbunge maalum John Mbadi ambaye ameteuliwa waziri wa fedha kwenye mabadiliko yaliyotangazwa na Rais William Ruto majuma mawili yaliyopita.

Kama sehemu ya kutunuku Kaunti ya Busia ambayo ni ngome yake ya kisiasa, Mbunge wa Funyula Oundo Mudenyo amepewa wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji Bungeni (PIC).

Hata hivyo, ODM bado haijajaza nafasi mbili za naibu kiongozi wa chama na pia ile ya uenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Bw Mbadi. Magavana wa zamani Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) ambao walikuwa wakihudumu kama naibu kiongozi wa ODM ni mawaziri wateule wa Madini na Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Ndogo.

Ubabe wa kisiasa hasa umeanza kushuhudiwa katika wadhifa wa uenyekiti huku mbunge wa Homa Bay Mjini Opondo Kaluma akisema wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Bw Mbadi lazima usalie Kaunti ya Homa Bay.

Hata hivyo, uteuzi wa Bw Mbadi kama waziri kisha Bi Odhiambo kama kiranja wa wachache, wote kutoka Homa Bay sasa unadidimiza matumaini ya nafasi hiyo kusalia katika gatuzi hilo.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo ambaye amekuwa akipigiwa upato kuwahi nyadhifa za Mwanasheria Mkuu au uenyekiti wa PAC, alitoka bure katika mabadiliko hayo.

Bw Amollo ambaye anatoka Kaunti ya Siaya sasa yupo pazuri kumrithi Bw Mbadi kama mwenyekiti wa ODM iwapo uongozi wa chama utaamua nafasi hiyo isalie Nyanza.