Habari za Kaunti

Mimba za matineja zaongezeka, wazazi wakidaiwa kula njama na washukiwa

Na OSCAR KAKAI July 26th, 2024 3 min read

ONGEZEKO la mimba, ndoa za mapema na ukeketaji limetajwa kama kizingiti kikubwa kwa elimu katika kaunti ya Pokot Magharibi licha ya juhudi za serikali na washikadau kuhakikisha kuwa maovu hayo yanakabiliwa.

Wasichana wenye umri wa miaka kati ya 12 na 18 ndio wameathirika zaidi huku wakiwacha shule kabla ya kufika darasa la nane.

Kaunti ya Pokot Magharibi ni ya pili nchini, na kiwango cha juu cha mimba za mapema kwa asilimia 36 na ukeketaji (44), kulingana na ripoti ya afya ya mwaka wa 2022 kutoka kwa taasisi ya Kenya National Bureau of Statistics (KNBS).

Mbinu za kupigana na mila potovu katika kaunti hii, zimekuwa hafifu na kufanya maovu hayo kuongezeka.

Hii inatokana na maisha magumu yanayochangia mimba za mapema kuathirika kiuchumi siku za usoni.

Kulingana na walimu, maovu haya yanatekelezwa na wanaume ambao tayari wako kwenye ndoa.

Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Holy Rosary, Consolata Sortum, alisema kuwa wasichana wengi hawasomi tena kwa kuwa wazazi wao ni kizingiti kwa kukomesha maovu haya kwani wanashirikiana na wanaume hao na kutatua kesi hizo kisiri nyumbani.

“Wasichana wengi wanapachikwa mimba na kupata magonjwa ya zinaa, suala ambalo huwafanya kuwacha shule,” akasema.

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Bakhita, Grace Kakuko, wanafunzi 25 hawakurejea shuleni kwa muhula wa pili kwani walishika mimba.

Bi Kakuko aliwataka wazazi kuchukua majukumu yao ya uzazi akisema kuwa wasichana wengi hupachikwa mimba wakiwa nyumbani.

Mwalimu huyo alisema kuwa kama walimu, wako tayari kuwapokea ili waweze kuendeleza elimu yao.

“Ninaomba machifu na viongozi kusaidia kusaka wasichana ambao wamepotea na kuwarejesha shuleni ,”akasema.

Mwalimu mkuu wa shule ya Sebit, Samuel Kapultin, alithibitisha kuwa wasichana watatu kwenye shule hiyo, tayari wamepata mimba tangu mwaka huu uanze.

“Mwaka jana, tulikuwa na msichana mmoja ambaye alifanya mtihani akiwa na mimba na mwaka huu, wapo watatu ambao wako na mimba. Watoto wengi hujitegemea kwa kuhusika na uchimbaji mawe,” akasema.

Imetambuliwa kuwa wasichana wengi katika maeneo ya mashinani hutoroka kutoka maovu hayo na kukosa usaidizi.

Mratibu wa shirika la Declares Kenya, Jefferson Mudaki, alisema kuwa mimba za mapema vimeshamiri katika Kaunti ya Pokot.

“Huu mwaka tulikuwa na visa vya mimba za mapema 8700. Tulifikiria kuwa visa hivyo vitapungua baada ya janga la Corona kuisha lakini bado vinaongezeka,”akasema.

Bw Mudaki alisema kuwa kuna haja serikali ya kaunti itenge fedha za mipango ya afya kwa uzazi.

“Miiko na mila potovu vimechangia mimba za mapema,”akasema.

Bw Mudaki alisema kuwa kuna changamoto ya kukosa sera za kumaliza maovu hayo.

“Hakuna sheria inayoleta washikadau kupigana vyema. Unapata wengine wanafanya kazi eneo moja la kusahau mengine,” akasema.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Kapenguria, Bw Mudaki aliongeza kusema kuwa vijana wanapata mafunzo kuhusu kufanya mapenzi ni changamoto kuu kwani wanaume wanabaki kuwa waamuzi kwa masuala ya kupanga uzazi.

“Mimba za mapema zimekuwa changamoto kuu kwani idadi ya watu inapanda tu .Hii ni jamii ya wafugaji na masuala ya ngono huwa hayajadiliwi peupe. Ni mwiko,”akasema.

Aliwatahadharisha viongozi dhidi ya kupeana habari za kupotosha na kuwataka wakazi kuzaa watoto wengi ili wapate kura.

“Wasichana wadogo huwa hawafanyi maamuzi yao ya kibinafsi, viongozi na wazee huwamulia. Tumekuwa tukihamasisha jamii na kupena habari kuhusu afya ya uzazi na mpango wa uzazi ili waelewe kuhusu masuala ya ngono. Tunajumuisha vijana kwenye mitandao, kuandika ujumbe na uhamasisho kupitia kwa vyombo vya habari,” akasema Bw Mudaki.

Afisa wa masuala ya afya ya uzazi katika kaunti ya Pokot Magharibi, Consolata Siree, alisema kuwa mimba za mapema kati ya wanafunzi inachangia athari za kiakili na masomo.

Kulingana na ripoti ya mwaka wa 2022 kutoka kwa National council for Nomadic Education in Kenya (NACONEK), kaunti hiyo ina watoto 42, 770 ambao hawako shuleni.

“Wadau wote wanafaa kuunga mkono juhudi za elimu na kuhakikisha kila mtoto anaenda shuleni,” akasema Bw Wamae.

Aliwataka machifu kusaidia kwa usajili wa watoto shuleni na kuipa elimu kupau mbele.

“Hatutaki mtoto yeyote kusema kuwa hakupewa nafasi ya kusoma. Tunataka warani wapate shahada. Katiba inampea kila mtoto haki ya kusoma,” akasema.

Bw Wamae aliwataka wakazi kukumbatia elimu na kupeleka wanao shuleni pamoja na kuwacha mila potovu.

“Huwezi kufanya maendeleo bila elimu,” akasema Bw Wamae.

Alisema kuwa serikali imeweka mikakati kuhakikisha kuwa kila mtoto anaenda shuleni.

“Tumejaribu kurejesha wanafunzi 3400 shuleni,” akasema.

Mzazi Jane Karipuka, alisema kuwa watoto wa eneo hilo wanahitaji ulinzi.

Msichana mwenye umri wa miaka 16 ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema kuwa wasichana wengi hawana uwezo wa kupata sodo.

“Mtu amabye yuko tayari kusaidia anataka ngono kabla akupee fedha za sodo ya mwezi mzima,” akasema msichana huyo.