Habari Mseto

Mimi na dadangu tunapanga kuolewa na mwanamume mmoja

January 1st, 2024 1 min read

Vipi shangazi? Mimi na dada yangu mdogo tumevutiwa kimapenzi na mwanamume mmoja na hakuna anayetaka kumuachia mwenzake. Sasa tumeamua kuolewa pamoja. Waonaje?

Sioni ubaya wowote kuhusu makubaliano yenu na hakuna anayeweza kupinga uamuzi huo. Hata hivyo mpango huo utafaulu tu iwapo mwanamume huyo yuko tayari kuoa wake wawili.

Mpenzi atishia kuniacha baada ya mama kumkataa

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili. Tunapendana sana na ameahidi kunioa. Lakini mama yangu amekuwa akipinga uhusiano wetu na sasa mwenzangu anatishia kuniacha kwa sababu hiyo. Naomba ushauri wako.

Ninaamini wewe ni mtu mzima na ni wajibu wako kuamua unachotaka maishani. Mama yako hana haki ya kuingilia uhusiano wenu. Jaribu kuzungumza na mpenzi wako umhakikishie kuwa uko tayari kuwa mke wake licha ya msimamo wa mama yako.

Bado siamini samaki amemeza chambo

Kwako shangazi. Mwanamke ambaye nimetamani kwa muda mrefu awe mpenzi wangu hatimaye amekubali. Sasa hofu yangu ni kuwa akitaka burudani nitashindwa kwani bado siamini ni mpenzi wangu.

Hatua unayofikiria kuchukua ni muhimu sana kwa mwelekeo wa uhusiano wenu. Akikubali ombi lako kisha ushindwe atafikiria humpendi na atakuacha. Ushauri wangu ni kuwa usubiri hadi upate ujasiri wa kutekeleza shughuli hiyo ipasavyo.

Aliyeniacha kanipigia simu juzi, eti ananipenda

Kwako shangazi. Nilikuwa na mpenzi lakini akaniacha akaolewa na mtu mwingine. Juzi alinipigia simu kunijulia hali na baadaye akanitumia ujumbe akisema bado ananipenda. Nampenda pia. Waonaje?

Mwanamke huyo ameamua kuvunja ndoa yake. Simu aliyokupigia haikuwa ya kukujulia hali. Alitaka kuungama penzi lake kwako kwa sauti yake lakini akashindwa. Badala yake akatuma ujumbe. Mtafute mzungumze.