Kimataifa

'Mishuto' yalazimisha polisi kuacha kuhoji mhalifu

October 23rd, 2018 1 min read

GEOFFREY ANENE NA MASHIRIKA

Mwanamume mmoja mhalifu, ambaye alitumia ‘mishuto’ kufanya mpelelezi kukatiza mahojiano, hatimaye amekiri makosa ya kumiliki bunduki na mihadarati.

Gazeti la The Kansas City Star nchini Marekani limeripoti kwamba Sean Sykes Jr, ambaye ana umri wa miaka 25, alikubali mashtaka Oktoba 22, 2018.

Alikamatwa katika kizuizi cha barabarani mwezi Septemba katika eneo la Kansas City, Missouri, ambapo maafisa wa polisi walimpata na begi la mgongoni lililokuwa na dawa na bunduki.

Sykes alikuwa abiria katika gari hilo. Kachero alisema kwamba alipoliuza Sykes anakotoka, “aliinua tako upande mmoja wa kiti alichokuwa amekalia na kutoa bomu la ushuzi kabla ya kupeana jibu.”

Stakabadhi za mahakamani zinasema kwamba Sykes “aliendelea kutoa makombora hayo” na kulazimu mpelelezi huyo kukatiza mahojiano yake kabisa. Sykes atahukumiwa baada ya ripoti ya kabla ya hukumu kukamilishwa.