Habari Mseto

Mjukuu wa Moi ashtakiwa kukosa kununulia watoto chakula

February 6th, 2024 1 min read

Na JOSEPH OPENDA

MJUKUU wa rais wa zamani Marehemu Daniel arap Moi yuko mashakani tena baada ya mke wake wa zamani kumshtaki tena kwa kukaidi agizo la mahakama lililomtaka kugharimia mahitaji ya watoto wao wawili.

Hakimu Mkuu wa Nakuru ameamuru kuwa Bw Collins Kibet Toroitich Moi aeleze ni kwa nini hafai kuadhibiwa kwa kukaidi maagizo ya mahakama.

Katika maagizo yaliyotolewa Juni 22, 2022, mahakama iliamuru kuwa Bw Kibeti agharimie karo ya shule ya watoto hao, matibabu na bili ya starehe yote ikigharimu Sh1.5 milioni kwa mwezi.

Hata hivyo, mkewe wa zamani Gladys Jeruto Tagi amerejea kortini akilalamika kuwa Kibet amedharau maagizo hayo.

Bi Tagi anadai kuwa mumewe wa zamani alitelekeza majukumu yake ya malezi na kumwachia mzigo huo. Mahakama iliambiwa kuwa Bi Tagi ndiye amekuwa akilipa karo na kugharimia bili za matibabu na burudani ya watoto hao hali ambayo imemsababishia changamoto nyingi za kifedha.

“Ingawa anafahamu majukumu yake ya malezi kama mzazi, mshtakiwa alifeli na kukataa kulipa karo na kulipia mahitaji mengineyo alivyoagizwa na korti,” akasema Bi Tagi kwenye stakabadhi za mashtaka aliyowasilisha kortini.

Mwanamke huyo anadai kutumia jumla ya Sh2.8 milioni za kugharamia mahitaji ya watoto hao kuanzia Juni 2, 2022 mahakama hiyo ilipotoa agizo hilo.