Habari za Kitaifa

Mkutano wa Kenyatta kuondoa chama cha Raila Azimio

Na CHARLES WASONGA August 19th, 2024 2 min read

BAADHI ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya sasa vimeanzisha kampeni inayolenga kufanikisha kuondolewa kwa ODM kutoka muungano huo baada ya Raila Odinga kuamua kufanya kazi na serikali ya Rais William Ruto.

Viongozi wa vyama vya; Wiper, Jubilee, DAP-K na PNU wamefichua kuwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ameitisha kikao ambacho kitatumiwa kupitisha pendekezo la kufurushwa kwa ODM na kuratibu mustakabali wa Azimio.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, viongozi hao wanashikilia kuwa ODM haifaa kuendelea kusalia ndani ya Azimio ilhali wanachama wake wanahudumu katika serikali ya Rais Ruto.

“Haitawezekana kwa ODM kuhakiki utendakazi wa serikali ilhali wanachama wake wanashikilia nyadhifa kuu za uwaziri katika serikali hiyo hiyo. Ingawa ni haki ya wenzetu kuamua kufanya kazi na serikali au mrengo wa upinzani, itabidi chama chao kuamua kusalia upinzani au kuwa sehemu ya serikali,” Bw Musyoka akasema Jumapili, Agosti 19, 2024 alipoandamana na wenzake kuhudhuria ibada katika Kaunti ya Kirinyaga.

“Suala hili ni miongoni mwa yale yatakayojadiliwa katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Azimio utakaoongozwa na mwenyekiti wetu Uhuru Kenyatta,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Musyoka hakutaja siku wala tarehe ya kufanyika kwa mkutano huo. Hata hivyo, duru zimeiambia Taifa Dijitali kuwa mkutano huo utafanyika wiki hii.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni ameisuta ODM kwa kuendeleza undumakuwili katika nyanja ya siasa na uongozi, hali aliyosema ni kinyume cha moyo wa Katiba ya sasa.

“ODM haiwezi kuwa ndani ya serikali na wakati huo huo inadai ingali katika upinzani. Hii ni kwa sababu wanachama wake wanashikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali hii ya William Ruto,” akasema Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua.

Bw Kioni alisema ODM imekosea kwa kushirikiana na serikali, ambayo kwa mtazamo wake, inanyanyasa Wakenya.

“Katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Azimio, tutataka ODM iondolewe Azimio ili tupate nafasi ya kuweka mikakati ya kuihakiki serikali hii ya Kenya Kwanza,” Bw Kioni akasema.

“Kwa kuvuta viongozi wa upinzani upande wake, Rais William Ruto ameonyesha wazi kuwa anapania kuendelea kuwadhulumu Wakenya. Hatuwezi kukubali kuendelea kwa mwenendo huo,” akaongeza.

Kiongozi wa DAP- Kenya Eugene Wamalwa alisema Rais Ruto anaendesha serikali inayokiuka Katiba kwa sababu inashirikisha viongozi wa upinzani bila kufuata mwongozo wa kisheria.

“Baraza la mawaziri lililoundwa juzi na Rais William Ruto sio halali kwa sababu halitambuliwi na Katiba yetu. Hili sio baraza la mawaziri chini ya serikali ya muungano, serikali ya mseto au ile inayofuata mifumo inayotambuliwa na sheria yoyote nchini au sheria za kimataifa. Kwa hivyo, hii sio serikali halali,” akasema Bw Wamalwa.

“Ikiwa wenzetu wa ODM wanataka kushirikiana na serikali kama hii, basi waondoke Azimio,” akaongeza Bw Wamalwa, ambaye mbunge wa zamani Saboti na aliyehudumu kama Waziri wa Ulinzi chini ya serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Migawanyiko ilianza kushuhudiwa katika muungano wa Azimio baada ya Rais Ruto kuteua viongozi watano wa ODM katika baraza lake jipya la mawaziri.

Walioteuliwa ni manaibu wa Bw Odinga; Wycliffe Oparanya na Ali Hassan Joho, aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani wa kitaifa John Mbadi, aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa James Opiyo Wandayi na alikuwa mwanachama wa Kamati Shirikishi ya Kusimamia Uchaguzi katika ODM Beatrice Askul Moe.