Habari za Kitaifa

Mudavadi anavyocheza karata yake ya kisiasa chini ya maji

April 16th, 2024 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi anajaribu kung’aa katika utawala wa Kenya Kwanza huku akiendesha mikakati ya kujiweka pazuri kisiasa kabla ya 2027 na kinyang’anyiro cha urithi wa urais 2032.

Baada ya kujiunga na siasa akiwa na umri mdogo wa miaka 29, mnamo 1989, kimsingi Mudavadi ndiye afisa mwenye tajriba kubwa zaidi katika serikali ya Rais William Ruto.

Isitoshe, Waziri huyo wa Masuala ya Kigeni amejijengea himaya ya sifa kama kiongozi asiye mbishi na mwenye mawazo pevu katika serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Mudavadi alijiuzulu wadhifa wake wa Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) mnamo Oktoba 2022 baada kuteuliwa mkuu wa mawaziri (PCS). Hii ni kulingana na hitaji la kipengele cha 77 (2) cha Katiba.

Bw Mudavadi amekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kufanikisha azma ya Rais Ruto kuhakikisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga anashinda wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Naibu huyo wa zamani wa Waziri Mkuu juzi aliwashangaza wafuasi wake alipodokeza kuhusu uwezekano wa kutokea kwa “tetemeko” jingine la kisiasa sawa na lililotokea alipojiunga na mrengo wa Rais Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Aidha, alidokeza kuhusu mpango mpya wa kukiimarisha chama cha United Democratic Alliance (UDA), na kuashiria kuhusu mipango ya kuvunjwa kwa ANC, ili wanachama wajiunge na chama hicho kinachoongozwa na Rais Ruto.

Jana, Taifa Leo ilielezwa kuwa asasi mbalimbali za chama cha ANC zimeanza “mazungumzo ya kina kuhusu mpango wa kujiunga na UDA,” ili kuandaa mwongozo kuhusu mchakato huo.

Baraza la ANC, lenye mamlaka ya kuendesha masuala ya kisiasa ya chama hicho, na asasi ya pili yenye ushawishi baada ya Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC), linatarajiwa kuanzisha mazungumzo kuhusu suala hilo “hivi karibuni.”

Kulingana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, muungano na mseto wa vyama viwili au zaidi vinaweza kuja pamoja kuunda chama kipya au chama kilichoko (kama vile UDA).

Hii ni baada ya chama hicho kufuata Katiba yake na taratibu za kufikia uamuzi kama huo wa kuungana na chama kingine.

Makubaliano ya muungano hutiwa saini na kuwekwa katika afisi ya msajili katika muda wa siku 21 baada ya kutiwa saini.

Hatua hiyo humfanya msajili kuondolea mbali cheti cha usajili wa vyama vya kisiasa vilivyoungana . Kisha kwa muda wa siku saba, ataweka kwenye gazeti rasmi la serikali tangazo kuhusu kuvunjwa kwa vyama hivyo.

Cheti cha usajili hutolewa kwa chama kipya cha kisiasa kitakachobuniwa na hivyo mwanachama wa chama kilichoungana na kingine, moja kwa moja, huwa mwanachama wa chama kipya.

Rais, Naibu Rais, Magavana, Maseneta, Wabunge na madiwani waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vilivyoungana wataendelea kushikilia nyadhifa zao hadi mihula yao itakapokamilika.

Kauli ya Mudavadi juzi kuhusu uwezekano wa ANC kujiunga na UDA imeibua hisia mseto, huku baadhi ya wanachama wa ANC wakipinga wazo hilo.

Katibu Mkuu wa ANC Omboko Milemba ambaye wiki jana aliwahakikishia wafuasi wa chama hicho kwamba hakitavunjwa, jana alionekana kubadili msimamo.

Alieleza kuwa alipinga pendekezo hilo kabla ya kushauriana na Bw Mudavadi ambaye ni mwanzilishi wa ANC kuhusu mipango ya siku zijazo na manufaa yatakayojiri.

“Nina uhakika kwamba atanipigia simu na tuzungumze kuhusu suala hili na mipango yake kwa sababu mimi ni mshirika katika mipango hiyo,” Bw Milemba ambaye ni Mbunge wa Emuhaya aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Akaongeza: “Wakati huu sijapata maagizo kuhusu suala hili; labda unafahamu mengi kunizidi. Hata hivyo, pindi nitakapopata maagizo, nitayawasilisha kwa uwazi.”