Habari za Kitaifa

Muheria akashifu wanasiasa fisadi na wenye kusema uongo kila wakati

February 15th, 2024 1 min read

Na JAMES MURIMI

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria, amewaonya wanasiasa dhidi ya kueneza ufisadi na kuwahadaa Wakenya wakati huu ambapo changamoto tele zinaendelea kuandama nchi.

Kiongozi huyo wa dini amewataka viongozi wote bila kuzingatia miegemeo ya kikabila, wamakinikie kutoa huduma kwa Wakenya badala ya kushiriki kwenye siasa ya ubabe na uporaji wa mali.

Akizungumza na wanahabari katika kanisa Katoliki la Our Lady of Consolata mjini Nyeri, askofu huyo alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kujitajirisha huku raia wa kawaida wakiteseka.

“Na mikono yetu itetemeke kabla hatujaingilia ufisadi na hadaa tupu. Tuwe tayari kuapa kuwa Mungu atulaani iwapo tutashiriki ufisadi.

Tuwe tayari kukabiliana na athari za kutumia nafasi za uongozi vibaya na kupata utajiri ambao ni wa Wakenya,” akasema Askofu Muheria.

Mtumishi huyo wa Mungu alilalamika kuwa baadhi ya Wakenya wamekuwa wakiwashangilia viongozi ambao wanatoa ahadi za uongo na wanafahamu vizuri hawawezi kutimiza ahadi hizo.

“Kwa sasa wanasiasa wetu wanashindana katika kusema uongo. Wananchi nao wamezoea kudanganywa na wanawashangilia viongozi ambao wanasema uongo. Inashangaza kuwa tunajifanya sisi ni Wakristo ilhali tumebobea katika kusema uongo na kutoa ahadi ambazo hatuzitimizi,” akasema Askofu Muheria.

“Lazima tuwe watu wa kusema ukweli na wa kuaminika. Namwomba Mungu abadilishe roho zetu ili tumakinikie mafunzo ya dini na tujifunze kusema ukweli. Wale ambao wanaongozwa na uchoyo nao tunawaomba wabadilike,” akaongeza.

Mwezi uliopita, Rais William Ruto alihakikishia nchi kuwa serikali, mahakama na bunge, zilikuwa zimekubaliana kuendeleza vita dhidi ya ufisadi kwa kuwatimua viongozi waliobobea kuchukua hongo.

“Nataka kuwaahidi Wakenya kuwa tuna umoja na lengo letu ni kuwaondoa wafisadi kutoka nchi yetu,” akasema Rais Ruto alipokuwa akifungua Taasisi ya Kiufundi na Teknolojia ya Gilgil, Kaunti ya Nakuru.