Makala

Nani anaua wanawake Nakuru? Hofu saba wakitolewa uhai ndani ya mwezi mmoja


HOFU imetanda kwa wakazi wa maeneo bunge ya Rongai na Bahati kaunti ya Nakuru kufuatia msururu wa mauaji yanayolenga wanawake na wasichana.

Huko Bahati, mwanafunzi wa kidato cha pili, Beauty Njeri, alinajisiwa na kuuawa akielekea shuleni mwezi uliopita.

Huko Rongai, wanawake hao wawili na msichana wa miaka mitano waliuawa  vivyo hivyo na miili yao kutupwa katika shamba la mahindi.

Wakazi wanajiuliza ni nani anaua wanawake na wasichana? Je, kuna genge la uhalifu linalolenga wanawake?

Mnamo Julai 15, Alice Ayuma Blessing mwenye umri wa miaka mitano alinajisiwa, akauawa na mwili kutupwa katika shamba la mahindi mita chache kutoka nyumbani kwao.

Wiki kadhaa baadaye, mvulana mdogo ambaye alikuwa akiwinda ndege shambani aliupata mwili wake na kuwafahamisha wakazi.

Mnamo Jumatano wiki jana, mwili wa Bi Florence Mueni Mwalimu, 34, mfanyakazi wa Benki mjini Nakuru, ulipatikana umetupwa katika shamba la mahindi karibu na nyumbani kwake katika kijiji cha Kalyet huko Rongai. Alikuwa amekatwa kichwa na vidole gumba vyake.

Pia alikuwa na majeraha makubwa ya kisu usoni na sikio lilikuwa limekatwa. Wenyeji walimwarifu chifu msaidizi wa eneo hilo ambaye aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Olrongai.

Ripoti ya uchunguzi wa  maiti ilifichua kuwa alikatwa sikio na vidole gumba vyake akiwa hai.

Inasemekana Bi Mueni aliripoti kazini kama kawaida Jumanne wiki jana.

Lakini, saa mbili baada ya kufika kazini, aliingia katika ofisi ya meneja na kuomba  ruhusa ili kumpeleka a mtoto wake hospitalini. Inasemekana  baada ya kupewa ruhusa,Bi Mueni alipakia vitu vyake na kuondoka benki. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho  kuonekana akiwa hai.

Kulingana na mumewe, Erick Mureithi, alipokea simu kutoka kwa mwanawe mwenye umri wa miaka 11 mnamo Jumanne saa 10 jioni akimjulisha kuwa mama yao hakuwa amefika nyumbani.

Alisema kuwa alijaribu kumpigia simu lakini ilikuwa imezimwa.

Baadaye alimpigia simu mamake Mueni ambaye alimweleza kwamba walizungumza mara ya mwisho  saa 11tano asubuhi baada ya kupiga simu kuuliza kuhusu kakake ambaye alikuwa amelazwa hospitalini.

Mureithi alisema alisafiri kutoka Kisii Jumatano na kuelekea benki kuulizia aliko mkewe.

Meneja wa benki alisema alikuwa ameondoka ofisini mapema. Hata hivyo, saa nane usiku, alipokea simu kutoka kwa chifu wa eneo hilo akimtaka aripoti katika Kituo cha Polisi cha Olrongai.

Baadaye alipelekwa eneo la tukio ambapo alithibitisha mke wake wa miaka 12  alikuwa ameuawa kikatili. Alisema kwa miaka  12 ya ndoa yao mkewe hakuwa ameeleza hofu yoyote kwamba maisha yake yalikuwa hatarini.

Siku moja baada ya mwili wa Mueni kupatikana, wakazi wa Baraka Estate waliupata mwili wa mwanamke katika shamba la mahindi karibu na reli.

Waliwaarifu maafisa katika Kituo cha Polisi cha Baraka.

Mwili huo ulitambuliwa baadaye kuwa wa Vella Moraa, 28, mkazi wa Mustard Seeds Estate, ambaye alikuwa ameripotiwa kutoweka siku moja  iliyopita.

Mwili wake ulipatikana mita 500 kutoka nyumbani kwake ukiwa na majeraha ya  kisu.

Mumewe, Elisha Otieno, 30, aliambia polisi kwamba mkewe, ambaye ni mchuuzi wa chakula, aliondoka nyumbani Jumatano kwa biashara yake ndani ya Baraka Estate lakini hakurejea nyumbani.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Moraa alibakwa na kudungwa kisu mara nyingi kichwani na usoni.

Maafisa wa upelelezi bado wanaendelea kuwasaka waliomuua msichana Beauty Njoki mwenye umri wa miaka 16, aliyeuawa mwezi uliopita.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya St John iliyopo Bahati aliuawa Juni 4 kikatili alipokuwa akielekea shuleni mwendo wa saa kumi na moja  asubuhi na mwili wake kutupwa kwenye kichaka.

Matukio hayo yamewaacha wakazi wa kaunti ndogo za Rongai na Bahati wakiishi kwa hofu kwa kuwa hakuna mshukiwa hata mmoja aliyekamatwa.