Siasa

Ndindi Nyoro awajibu wandani wa Gachagua

June 2nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro amewajibu wandani wa Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua ambao wamekuwa wakimsuta katika mikutano ya umma kwa madai kwamba anatumika kusambaratisha umoja wa Mlima Kenya.

Bw Nyoro sasa amesema kwamba eneo la Mlima Kenya limegeuka kuwa soko la domo la siasa huku wananchi wakiachwa kwa mataa katika huduma za kiutawala.

Akiongea katika Kaunti ya Kakamega mnamo Mei 31, 2024, mbunge huyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa alisema kwamba “tunafaa tuelewe kwamba wananchi wetu hawana haja na maneno matupu na ya ovyo, kile kinachowasumbua ni huduma”.

Majibu ya Bw Nyoro yameingia siku moja tu tangu Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu kuteta kwamba “kuna wandani wa Bw Gachagua kama mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya—ambaye ni mzawa wa eneobunge la Kigumo katika Kaunti ya Murang’a—na mbunge wa zamani wa Bahati Bw Kimani Ngunjiri ambao wamekuwa wakimtajataja Bw Nyoro kwa kumwekea lawama zisizoeleweka”.

Bw Nyutu aliteta kwamba “sawa na jinsi wanavyotaka Bw Gachagua aheshimiwe, nao wamheshimu Bw Nyoro na wakome kumtajataja ovyoovyo wakimwekelea maneno ambayo hayana msingi wowote”.

Akihutubu, Bw Nyoro alisema kwamba “sisi katika serikali tunafaa tuungane kwa kuchapa kazi kwa manufaa ya mwananchi kwa kuwa mafanikio yetu hayatatokana na domo tulilo nalo lakini yatazuka kutoka kwa matendo”.

Aliongeza kwamba kwa sasa kiongozi wa nchi – Rais William Ruto akishirikiana na Bw Gachagua, wanaongoza taifa ambalo linahitaji maendeleo wala si domo “na sisi tulio chini yao katika nyadhifa nyingine zote tunafaa kuwajibikia matendo ya kuinua maisha ya Wakenya wala si kuwachokesha masikio na bongo kwa maneno matupu”.

Alisema mashujaa wa mataifa ambayo yamefanikiwa kuimarika kimaendeleo kama wasomavyo katika historia hawakumbukwi na kurejelewa kwa msingi wa maneno waliyotoa katika majukwaa bali ni kupitia matendo yao ya kuchangia uchumi kuinuka.

Alitoa mfano wa Rais wa Tatu, marehemu Mwai Kibaki ambaye anasifika kwa kuinua uchumi wa Kenya katika awamu yake ya kati ya 2002 na 2013.

“Ukiuliza Wakenya kuhusu aliyoongea hawawezi wakayakumbuka lakini wanakumbuka jinsi alivyoimarisha uchumi wa Kenya,” akasema.

Bw Nyoro licha ya kuwa hajanukuliwa akisema kwa mdomo wake, ni mmoja ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akisemwa kuwa miongoni mwa wanaomezea mate wadhifa wa Bw Gachagua katika uchaguzi mkuu wa 2027 na pia urithi wa ikulu 2032.

Seneta Nyutu amekuwa akimpigia debe katika ukanda wa Mlima Kenya, hali hiyo ikiamsha joto la kisiasa eneo hilo kiasi kwamba wandani wa Bw Gachagua nao wamekuwa wakimkemea Nyoro hadharani katika simulizi kuhusu wale wanaotambulika kama wasaliti wa umoja wa kijamii.

Bw Nyoro, Mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri na Gavana wa Nairobi Bw Johnson Sakaja ni miongoni mwa wale ambao wamekuwa wakilengwa kwa kiwango kikuu na wandani wa Bw Gachagua.

Tayari, Bw Kiunjuri amemjibu Bw Gachagua akimtaka akome kuchochea wandani wake kukosea heshima wengine na kuwadunisha kwa kuwabandika majina ya dharau.

Bw Sakaja aidha amemsuta Bw Gachagua kama mkorofi na ambaye amekuwa akihangaisha baadhi ya viongozi wengine kwa miaka miwili hadi sasa.

Akimtaja kama mwoga, Bw Sakaja alimtaka Bw Gachagua kuheshimu nyadhifa za wengine kwa kuzingatia kwamba si eti wengine walipewa vyeo vyao bila ya kuchaguliwa.

“Hata sisi tulichaguliwa, si eti tulipewa nyadhifa hizi…kwa hivyo ni vyema hata nasi tuheshimiwe kwa kuelewa kwamba kutudharau ni kama kuwadharau wapigakura wetu waliotuaminia nyadhifa zetu,” Bw Sakaja akafoka.