Habari za Kitaifa

Niko ngangari kabisa kuongoza nchi, Ruto asema

Na WAIKWA MAINA July 14th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto amesema yuko imara kwenye uongozi wa serikali yake na kwamba changamoto zinazomkabili sio pigo kwa utawala wake, bali ni mwamko mpya wa kuwa kiongozi bora kutokana na aliyojifunza.

Kiongozi wa Taifa alisema haya Jumapili katika Kaunti ya Nyandarua ambapo alihudhuria Ibada ya kanisa.

“Nimeshika usukani kikamilifu, niko imara zaidi, nawahakikishia Wakenya nitakuwa na baraza bora zaidi la kuwahudumia Wakenya. Ninaendea serikali ya umoja kitaifa, mniombee, utawala wangu umejitolea kuipeleka Kenya mbele,” Rais Ruto.

Ibada hiyo ilifanyika kilomita chache kutoka Shule ya Msingi ya Ndururi ambapo wiki chache zilizopita, Rais alikumbana ana kwa ana na wanarika wa Gen Z waliokuwa wanaandamana na kulazimu kikosi chake cha usalama kumwondoa upesi.

Huku akiahidi kufadhili kukamilisha ujenzi wa Kanisa la Ndogino AIPCA, Rais alisema marufuku dhidi ya hafla za kuchangisha pesa kanisani itaathiri vibaya miradi ya kanisa.

Rais William Ruto akizungumza na wenyeji wa Nyandarua, Jumapili. Picha|Bonface Mwangi

Alisema sheria hiyo itapitishiwa mchakato wa kuwashirikisha Wakenya ili waidhinishe na kutoa maoni kuhusu jinsi viongozi watakavyoendelea kufadhili miradi ya kanisa.

“Naagiza Naibu wangu wa Rais Rigathi Gachagua na uongozi wa kanisa kutathmini ni kiasi kipi kinahitajika kukamilisha kanisa ili niandike hundi,” alisema Dkt Ruto.

Rais alisema amefanyia mabadiliko Huduma ya Polisi Nchini ili kuhakikisha utendakazi bora akisema vita dhidi ya ulevi vinapaswa kupatiwa kipaumbele kote nchini.

Alisema awali kulikuwa na utata kuhusu iwapo Nyandarua ni Eneo la Kati au Bonde la Ufa.

Alisema miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na serikali yake itakamilishwa, ikiwemo vituo vitatu vya soko vyenye thamani ya Sh200 milioni, alivyosema vitakamilishwa kufikia mwaka ujao.

Naibu Rais Gachagua alilalamika kuwa Nyandarua ilitelekezwa na kusahauliwa na utawala uliotangulia, na kumsihi Rais kuwa na hazina ya kina mama na vijana Nyandarua.

Alisema anamuunga mkono Rais na kumrai bosi wake kuwateua watu wanaofaa katika baraza.

“Sasa una fursa murwa ya kuunda baraza bora linalowaheshimu Wakenya, linaloelewa kuwa Wakenya ndio waajiri wetu, na wanastahili huduma bora, ukiteua baraza bora tutakuunga mkono kufanikisha na kutimiza agenda yako ya maendeleo,” alisema Bw Rigathi.