Habari za Kitaifa

Pigo kwa Gachagua wabunge 14 wa Mlima Kenya wakisema Kindiki tosha

Na GEORGE MUNENE September 10th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amepata pigo kubwa kisiasa katika ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya baada ya wabunge 14 kumwidhinisha Waziri wa Usalama Kithure Kindiki kama msemaji wao.

Wabunge hao wanatoka kaunti za Tharaka Nithi, Embu na Meru, zilizoko eneo la Mlima Kenya Mashariki.

Hatua hiyo sasa imegawanya eneo pana la Mlima Kenya kisiasa, haswa kwa misingi ya urithi wa kisiasa.

Wakiongea na wanahabari baada ya kufanya mkutano wa faraghani katika mkahawa wa Isaak Walton, Embu, wabunge hao 14 Jumatatu walitangaza kuwa Profesa Kindiki ndiye atakuwa kiunganishi kati ya serikali ya Rais William Ruto na eneo la Mlima Kenya Mashariki.

Hii ina maana kuwa Profesa Kindiki anasukumwa kuhujumu azma ya Bw Gachagua ya kuunganisha kisiasa eneo pana la Mlima Kenya lenye jumla ya kaunti 10 pamoja na kaunti ya Nakuru iliyoko katikati ya Bonde la Ufa.

“Tumekubaliana kwa kauli moja kwamba ngazi kati yetu na serikali ni Profesa Kindiki, eneo la Mlima Kenya Mashariki linainuka,” akasema Mbunge wa Mbeere Kaskazini aliyesoma taarifa kwa niaba ya wenzake.

Wabunge hao walisema wameungana kutetea maendeleo katika eneo la Mlima Kenya, wakiapa kutopumzika.

Walisema ipo haja kwa wao kushirikiana na Serikali ili kuharakisha ajenda za maendeleo Mlima Kenya Mashariki.

“Tuko na uhakika kwamba kupitia ushirikiano na mazungumzo na Serikali, eneo la Mlima Kenya Mashariki litawekwa katika ajenda ya maendeleo kitaifa,” wakasema.

“Mkutano huo ulikuwa hatua muhimu katika kuweka pamoja juhudi za pamoja za kuleta ustawi kwa manufaa ya watu wetu katika kaunti za Embu, Tharaka Nthi na Meru,” wakasema.

Wabunge wengine waliohudhuria mkutano huo ni; Nebart Muriuki (Mbeere Kusini), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki), Gitonga Murugara (Tharaka), Dan Kiiri (Igembe ya Kati), John Paul  Mwirigi ( Igembe Kusini), Mugambi Rindikiri (Buuri), Julius Taitumu (Igembe Kaskazini), Munene Parto (Chuka Igamba Ng’ombe) , John Kanyuithia (Tigania Magharibi) na Kareke Mbiuki ( Maara).

Wengine walikuwa; Njoki Njeru (Mbunge Mwakilishi wa Embu), Elizabeth Kailemia (Mbunge Mwakilishi wa Meru) na Seneta wa  Embu Alexander Mundigi.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga