Habari

RAILA AHEPWA: Wabunge wa ODM wasema 'Ruto Tosha 2022'

June 19th, 2018 2 min read

MOHAMED AHMED na VALENTINE OBARA

WABUNGE waasi wa Chama cha ODM katika eneo la Pwani, Jumatatu walihepa mkutano wa wabunge wa chama hicho na Kamati Kuu ya Kitaifa uliosimamiwa na kiongozi wao Raila Odinga mjini Mombasa.

Idadi kubwa ya wabunge hao wamekuwa wakihudhuria mikutano ya Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo siku za majuzi, na baadhi yao hata kutangaza watamuunga mkono kuwania urais 2022.

Miongoni mwa wabunge waliokosa kuhudhuria mkutano na ambao wamekuwa mstari wa mbele kumpigia Bw Ruto debe ni Aisha Jumwa (Malindi), Suleiman Dori (Msambweni), Badi Twalib (Jomvu), Benjamin Tayari (Kinango) na Owen Baya (Kilifi). Wengine ni Paul Katana (Kaloleni), Jones Mlolwa (Voi), Danson Mwashako (Wundanyi) na Seneta wa Taita Taveta Jones Mwaruma.

Hata hivyo, Gavana wa Kilifi Amason Kingi, ambaye pia amekuwa akihudhuria hafla za Bw Ruto na kumsifu kama kiongozi pekee anayeweza kutatua matatizo ya Wapwani, alihudhuria mkutano wa jana na akaketi karibu na Bw Odinga.

Bw Odinga alinuia kutumia mkutano huo kufafanua kuhusu ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta na kuwaomba wanachama kuunga mkono muafaka wa kuleta mabadiliko yatakayonufaisha wananchi wote. Hata hivyo, alisema mkutano huo haukutokana na hofu kwamba Bw Ruto anapenya katika ngome za ODM kutafuta umaarufu kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Lazima tukatae kupotoshwa na siasa za urithi na tuweke mawazo yetu katika ujenzi wa taifa jipya, kabla nafasi hii tuliyopata ipotee. Ni jukumu letu kufanya vipofu na viziwi wa kisiasa wasikie na kuona kwamba Kenya inabadilika na lazima watuondokee njiani,” akasema.

Duru zilisema kuna mipango ya kumpokonya Bw Dori wadhifa wa kusimamia Kundi la Wabunge wa Pwani kufuatia msimamo wake wa kumpigia debe Bw Ruto huku akitilia doa uwezo wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwa rais.

Duru kwenye mkutano wa jana zilisema Bw Kingi aliwaeleza wanachama kuhusu ushirikiano wake na Bw Ruto ambao awali alikuwa amesema ni hali ya kufuata nyayo za kiongozi wake wa chama alivyoungana na rais.

Wabunge zaidi ya 30 na maseneta wa ODM walihudhuria mkutano huo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Edwin Sifuna, alisema wanachama ambao walikosa kuhudhuria mkutano huo watapewa nafasi kueleza sababu zao kabla iamuliwe kama watachukuliwa hatua za kinidhamu. “Wataitwa ili wajieleze katika mkutano ujao. Tutawaarifu kuhusu hatima yao tutakapokuwa tayari,” akasema Bw Sifuna baada ya mkutano.

Wiki iliyopita, Bw Odinga alikosoa ziara nyingi za Bw Ruto katika maeneo mbalimbali ya nchi na kusema inafaa viongozi wawe wanahudumia wananchi badala ya kuzurura. Matamshi hayo yalikashifiwa vikali na viongozi wa Jubilee kutoka eneo la Kati ambao walimtetea Naibu Rais.