Habari Mseto

Ruto kuzuru Taita Taveta wakazi wakisubiri atimize ahadi za serikali yake

Na LUCY MKANYIKA July 27th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto anatarajiwa kuzuru Kaunti ya Taita Taveta Jumapili, huku ahadi za miradi aliyoahidi wakati wa ziara yake ya Oktoba mwaka jana zikisalia ndoto.

Katika ziara yake, Bw Ruto atashiriki ibada katika kanisa la Kianglikana la St Peters Bura Station lililoko katika eneo la Mwatate.

Ziara ya Rais inakuja huku miradi mbalimbali iliyokuwa miongoni mwa ahadi zake hata wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita zikiwa zimekwama huku wananchi na viongozi wakiitaka serikali kuzitimiza.

Wakati wa kampeni yake, Bw Ruto alizuru kaunti hiyo mara nyingi na kutoa ahadi kadha wa kadha kwa wakazi, kuanzia usambazaji wa maji, ujenzi wa barabara, ufufuaji wa reli ya zamani, ukamilishaji wa ujenzi wa uwanja wa ndege, miongoni mwa ahadi zingine.

Miongoni mwa miradi iliyokwama ni mradi wa bomba la pili la Mzima, ujenzi wa barabara ya Bura-Mghange-Mbale-Mtomwagodi pamoja na ile ya Taveta-Illasit.

Wakati wa ziara yake mwaka jana, Rais aliahidi kuwa mradi wa maji ya Mzima ungeanzishwa kufikia Disemba mwaka huo.

Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, aliyekuwa waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira Bw Zachary Njeru alisema kuwa serikali ilifutilia mbali mradi huo wa maji uliotarajiwa kugharimu takriban Sh35 bilioni ili kutafuta mbinu mpya ya kuutekeleza.

Vilevile, Rais aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha kuwa kaunti hiyo inapata asilimia 50 ya mapato ya hifadhi ya Tsavo.

Seneta Jones Mwaruma alisema kuwa ziara za Rais hazina faida kwa wenyeji wa eneo hilo.

“Sidhani ziara yake itaongeza thamani yoyote kwa wakazi wa Taita Taveta. Ningehudhuria kama angekuwa anazindua au kufungua miradi iliyokamilika baada ya miaka miwili akiwa uongozini,” alisema.

Bw Mwaruma alisema kuwa Rais ametelekeza Kaunti hiyo ambayo imesalia nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.

Miradi mingine, kama vile ule wa usindikaji wa mifugo ulioko katika eneo la Bachuma na ule wa uwanja wa ndege wa Ikanga iliyoko katika kaunti ndogo ya Voi ingali bado haijamalizika licha ya kugharimu mamilioni ya pesa.

Miundombinu katika mradi wa Bachuma uliogharimu takriban Sh380 milioni inaharibika licha ya kusalia mikakati michache ili kituo hicho kunufaisha wafugaji kutoka kote nchini.

Wananchi wanahisi kuwa serikali zilizopita na ile ya sasa zinawachezea shere kwa kushindwa kutekeleza miradi hiyo muhimu.