Habari za Kitaifa

RUTO NI YULE YULE: Rais arudia hali yake ya kawaida

Na COLLINS OMULO July 18th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto ameonekana kurejelea shughuli na hulka yake ya kawaida huku vijana wakiendeleza wimbi jipya la maandamano ya kupinga serikali yake.

Rais amekuwa akizuru kaunti mbalimbali katika maeneo ya Bonde la Ufa na Kati, kuzindua na kukagua miradi kadhaa ya maendeleo huku akiahidi kuchangia makanisa pesa.

Akiwa katika ziara hizo, Rais Ruto alijiepusha kuzungumzia suala la mazungumzo ya kitaifa ambayo yalipaswa kufanyika wiki hii kujadili yaliyoibuliwa na vijana waandamanaji.

Haijulikani ikiwa mazungumzo hayo yatafanyika au la baada ya baadhi ya vinara wa Azimio la Umoja kupinga wazo hilo. Dkt Ruto alizuru kaunti za Nyandarua na Nakuru alikofeli kutimiza baadhi ya ahadi alizotoa kwa vijana wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais alihutubia wananchi kando ya barabara, akazindua soko jipya katika Kaunti ya Nakuru, akakagua ujenzi wa kituo cha mabasi utakaogharimu Sh280 milioni na soko jingine litakalogharimu Sh300 milioni linalojengwa mjini humo.

Dkt Ruto pia alitangaza kurejeshwa kwa mpango wa ajira kwa vijana almaarufu “Kazi Mtaani” ambao ulianzishwa na mtanguliza wake Uhuru Kenyatta, lakini akaufutilia mbali Oktoba 2022.

Aidha, alidai kuwa shirika moja lisilo la kiserikali lenye makao yake nchini Amerika ndilo linadhamini maandamano ya kupinga serikali yake.

“Wale wanafadhili fujo, tunawajua. Nawalaani wale wanaohusika na machafuko yanayoshuhudiwa nchini. Aibu kwao!” akasema alipokuwa akiwahutubia wananchi katika eneo la Keringet, eneobunge la Kuresoi Kusini.

Kauli hiyo ilikuwa tofauti na ile aliyotoa alipokuwa akitangaza mipango ya mazungumzo yatakayoshirikisha wadau mbalimbali kujadili masuala yaliyoibuliwa na vijana hao wa Gen-Z wakati wa maandamano yao.

Rais Ruto alisema mazungumzo hayo ya siku sita, ambayo yaliratibiwa kuanza Julai 15 hadi Julai 20, 2024, yangetoa mwelekeo kuhusu mustakabali wa nchi.

“Tumekubaliana kwamba sharti tulete nchi hii pamoja. Hiyo ndiyo maana tumeitisha mdahalo utakaoshirikisha watu 150, kati yao 50 wakiwa vijana huku wengine 100 wakitoka makundi ya kidini, mashirika ya kijamii, vyama vya kisiasa na makundi ya wataalamu,” akasema Dkt Ruto.

Awali, alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa vijana katika majukwaa ya mtandao wa X, Rais pia aliomba msamaha kwa kutotilia maanani masuala yaliyoibuka kama vile ufisadi na utepetevu wa mawaziri.

Kiongozi wa taifa aliahidi kusikiliza masuala ya vijana, ambayo alisema ni yenye mantiki.

Alisalimu amri kutokana na presha za vijana alipokataa kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na kuvunja baraza lake la mawaziri.

Lakini baadaye, juma hili, serikali ya Dkt Ruto iliongeza kisiri ada ya utunzaji barabara kwa Sh7, kutoka Sh18 hadi Sh25 kwa lita ya mafuta aina za petroli na dizeli. Nyongeza hiyo ilijumuishwa katika bei mpya ya bidhaa hizo za petroli zilizotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta Nchini (EPRA) Jumatatu.