Habari za Kaunti

Sababu ya wanafunzi wengi kuingia shuleni Lamu bila hofu ya Al-Shabaab

Na KALUME KAZUNGU August 31st, 2024 1 min read

KUIMARISHWA kwa hali ya usalama katika vijiji vya Lamu vilivyoshuhudia mashambulio ya magaidi wa Al-Shabaab miezi kadhaa iliyopita, kumechangia idadi kubwa ya wanafunzi wanaohudhuria masomo muhula wa tatu ulipofunguliwa juma hili.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi madarasani katika shule mbalimbali.

Hizi ni shule zilizoko kwenye maeneo yaliyoshuhudia mashambulio yaliyolazimu familia kutoroka makwao.

Miongoni mwa shule, hasa zile za msingi za Lamu zilizoko maeneo yaliyovamiwa na Al Shabaab na ambazo zimejaa wanafunzi madarasani, ni Juhudi, Salama, Holy Angels, Majembeni, Mikinduni, Mavuno, Poromoko, Pandanguo, Witu na viunga vyake.

Mahudhurio asilimia 90

Katika mahojiano na Taifa Leo Ijumaa, wasimamizi wa shule hizo walikiri kushuhudia idadi kubwa ya wanafunzi waliohudhuria masomo, ikiwa imezidi asilimia 90.

Mwalimu Mkuu Wa Shule ya Msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi, Bw Amos Mithamo, aliishukuru serikali kuu kwa juhudi zake katika kudhibiti usalama wa vijiji vyao.

Shule ya Juhudi Primary imekuwa ikitumika sana kama kambi ya wakimbizi wakati vijiji vya maeneo hayo vinaposhuhudia uvamizi na mauaji yanayotekelezwa na Al-Shabaab.

Zaidi ya familia 500 kutoka vijiji mbalimbali zimekuwa zikipiga kambi shuleni humo kabla ya kufurushwa kurudi makwao Januari 2024 baada ya usalama kuimarishwa.

Hata hivyo kuna familia takriban 20 ambazo bado hupiga kambi shuleni Juhudi kila jioni inapoingia, ambapo hulala usiku kucha na kurudi makwao alfajiri.

Bw Mithamo alisema kambi za jeshi la KDF na polisi wa kukabiliana na dharura (RDU) maeneo yao, zinawapa matumaini wazazi wengi, hivyo kuwafanya kuwa huru kuachilia watoto wao kuhudhuria masomo kinyume na awali.