Makala

Sababu za watoto wa mpango wa kando kurithi mali yako

Na BENSON MATHEKA September 7th, 2024 2 min read

WATOTO wa mpango wa kando ambao mwanamume alikubali kuwa wake au aliokuwa  akitunza akiwa hai wanaruhusiwa kurithi mali yake.

Hawa ni watoto ambao mwanamume anazaa nje ya ndoa ambao alikubali kuwa ni wake au wale ambao alikubali kuwajibika kikamilifu ambao pia wanatambuliwa kama watoto wake chini ya sheria ya watoto.

Hapa, ni muhimu kuelewa kwamba watoto hao wanaweza kurithi mali ya marehemu mradi tu aliwatambua kama watoto wake.

Ni muhimu kufahamu kuwa mtu hawezi kurithi mali ya mtu aliyeua.

Sheria ya urithi ya Kenya inasema kwamba mtu aliye na akili timamu akiua mwingine, hawezi kurithi mali ya marehemu ima moja kwa moja au kupitia mtu mwingine.

Hii inamaanisha kuwa, mtu akiua baba yake kwa sababu ya mali, hata watoto wake hawawezi kurithi mali ya babu yao kwa niaba yake.

Sheria inasema kuwa mtu hafai kunufaika na vitendo vyake vilivyo kinyume cha sheria.

Ukiua mtu ukilenga kunufaika na mali yake, wakati wa kugawa mali hiyo, huwa inachukuliwa kuwa muuaji alitangulia kufa kabla ya mwathiriwa.

Hata hivyo, ni lazima tu apatikane na hatia ya kuua marehemu kwa sababu ya kumezea mate mali.

Hivyo basi, hauwezi kusingizia mtu mauaji ili kumnyima urithi, ni lazima mchakato wa sheria ufuatwe kikamilifu.

Mtu akifariki bila mke au watoto, mali yake huwa inarithiwa na jamaa zake wa karibu walio na uhusiano wa damu kuanzia kwa baba na iwapo alifariki mama iwapo angali hai. Iwapo wazazi wote hawapo, mali ya mtu akifariki bila mke na watoto huwa inaenda kwa ndugu zake na watoto wao.

Ndugu wanaorithi mali ya kaka au dada yao akifariki dunia bila mume au mke halali, huwa inagawanya kwa usawa baina yao. Iwapo ndugu wa kuzaliwa hawapo, mali hiyo huwa inamilikiwa na ndugu wa kambo na watoto wao na iwapo hawapo, basi inawafaidi watu wa karibu wa familia.

Sheria ya urithi inasema mtu aliye na wake wengi akifariki, mali yake huwa inaganywa kwa kila nyumba kwa kuzingatia idadi ya watoto na mama yao. Kwa mfano, iwapo A alikuwa na wake wawili X na Y huku X akiwa na watoto watatu na Y watoto 4, mali yake itagawanywa kwa watu 9 kwa kuhesabu watoto wa kila nyumba na mama yao