• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Atwoli ataka Duale apokonywe kazi

Atwoli ataka Duale apokonywe kazi

Katibu Mkuu wa COTU Bw Francis Atwoli. Picha/ Maktaba

Na BERNARDINE MUTANU

Kwa Muhtasari:

  • Bw Francis Atwoli asema Bw Duale alipotosha umma alipomuuliza Ukur Yattani hatua ambayo angemchukulia
  • Bw Atwoli alimkumbusha Bw Duale matukio ya awali ambapo mgogoro mkubwa ulishuhudiwa 2013
  • Asema wanachama wa COTU-K wana uhuru wa kumchagua wanayemtaka

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi (COTU) Francis Atwoli ametaka Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale afutwe kazi.

Katika taarifa ya Jumamosi, Bw Atwoli alisema Bw Duale alipotosha umma alipouliza waziri mteule wa Leba Ukur Yattani hatua ambayo angemchukulia Bw Atwoli ikiwa angepewa wadhifa huo.

Bw Atwoli ni mwanachama wa Bodi ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), ambayo iko chini ya Wizara ya Leba.
Akijibu, Bw Yattani alisema shughuli ya kwanza ikiwa atapewa wadhifa huo itakuwa kumwondoa Bw Atwoli na Bi Jacquelyn Mugo, anayesimamia shirikisho la waajiri (FKE) katika Bodi ya NSSF.

“Inasikitisha kuwa Kiongozi wa Wengi Bungeni anategemea tetesi kufanikisha majukumu yake. Yafaa aondolewe ili atakayepewa nafasi hiyo awe anaelewa sheria ili awe na uwezo wa kushauri bunge kwa njia inayofaa kuhusiana na suala muhimu kama hilo,” alisema Atwoli katika taarifa.

Awali, kulikuwa na mzozo kati ya wanachama wa Bodi ya NSSF na aliyekuwa Waziri wa Leba Kazungu Kambi ambao ulisuluhishwa na Waziri Raychelle Omamo 2015, alipokuwa kaimu waziri wa Leba baada ya Kazungu Kambi kufutwa kazi.

Kauli ya Bw Duale imefufua makovu kwani katibu huyo alimpuzilia mbali katika taarifa kali iliyotumwa katika vyumba vya habari jana.

“Kauli ya Kiongozi wa Wengi Bungeni ni ishara wazi kuhusiana na jinsi baadhi ya watu walioko mamlakani walivyo na tamaa kuu kuhusiana na uendeshaji wa NSSF,” alisema Bw Atwoli.

Katika taarifa hiyo, Bw Atwoli alimkumbusha Bw Duale matukio ya awali ambapo mgogoro mkubwa ulishuhudiwa 2013, baada ya Bw Kambi kufanywa Waziri wa Leba.

Kulingana naye, aliteuliwa kuhudumu katika NSSF akiwa na Bi Mugo kupitia kwa notisi katika Gazeti la Serikali Septemba 16, 2015 na Bi Omamo, baada ya msururu wa kesi mahakamani.

Bw Atwoli alisema mgogoro ulioshuhudiwa ulitokana na Bw Kazungu kutofuata sheria, zaidi ya kupuuza agizo la mahakama la kutoingilia shughuli za NSSF.

Alisema wanachama wa COTU-K wana uhuru wa kumchagua wanayemtaka kuwawakilisha katika bodi ya NSSF na kuongeza kuwa muhula wao wa kwanza kuhudumu katika bodi hiyo hajakamilika, na kwamba bado kuna muhula mwingine wa kuhudumu.

You can share this post!

Familia yakabiliwa na mzigo wa kulipia upasuaji wa binti ...

Wanafunzi 400 wenye funza wanufaika

adminleo