Masharti ya Oburu kwa Ruto kujiunga na ODM
KAIMU KIONGOZI wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, amekaribisha pendekezo la baadhi ya wanachama wa chama hicho kutaka Rais William Ruto arejee ODM, lakini akasema hilo lina masharti.
Dkt Oginga alisema iwapo Rais Ruto ataamua kuachana na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga tena na ODM, anapaswa kuelewa kwamba hatakuwa mgombea wa urais moja kwa moja, bali atapaswa kupambana na wagombeaji wengine watakaotaka nafasi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano na Runinga ya Ramogi Jumanne usiku, Dkt Oginga alisema ODM inalenga kuwa chama chenye nguvu zaidi kufikia mwaka 2027, na kwamba kitapendekeza mgombea wake wa urais kwa lengo la kuunda serikali ijayo.
“Tunataka ODM iwe chama imara, ili wanaotaka kujiunga nasi wakubali masharti yetu. Ikiwa Ruto ataona chama chetu kina mvuto, anaweza kurejea kwani ni mmoja wa waanzilishi wake. Lakini lazima awe tayari kushindana na wengine,” alisema Dkt Oginga.
Aidha, Dkt Oginga aliwataka viongozi wa zamani wa chama hicho “kuachia vijana” ambao wamekuwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, akisema wao ndio wanaopaswa kuendeleza urithi wake wa kisiasa.
“Viongozi wenzangu wa umri wa Raila wanapaswa kustaafu naye. Nafikiri kizazi kijacho, ambacho kilikuwa karibu naye, ndicho kinachopaswa kushika usukani,” alisema.
Aliongeza kuwa uongozi wa jamii ya Waluo hautakuwa mikononi mwa wanasiasa wa kizazi cha Raila, bali vijana wenye nguvu, maarifa na ari ya kuimarisha ODM kuelekea uchaguzi wa 2027.Dkt Oginga alifichua kuwa alishangaa kuteuliwa kuwa kiongozi wa muda wa ODM, akisema alijua kuhusu uteuzi huo kupitia Kiongozi wa Wachache Bungeni, Junet Mohamed, alipokuwa Kasarani.
Alisisitiza kwamba kiongozi wa jamii huwa ni mmoja kwa wakati, na kwamba atatokea miongoni mwa waliokuwa karibu na Raila.Katika juhudi za kuunganisha chama, Dkt Oginga alisema tayari ameanza kuzungumza na Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, kumhakikishia kwamba mchujo wa mgombea ugavana wa Nairobi utakuwa wa haki.
“Nasikia Babu ana wasiwasi kuwa atapokonywa tiketi ya ODM. Akishinda kura ya mchujo, atakuwa mgombea wetu. Sitaki aondoke chamani kwa hofu zisizo na msingi,” alisema.
Aliongeza kuwa amezungumza pia na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, ambaye licha ya wakati mwingine kutoa matamshi makali, bado ni mwanachama thabiti wa ODM.
Dkt Oginga alikiri kuwa chama kina changamoto katika maeneo ya Kakamega, Busia, na Nyando, na akasema anafanya kazi kuzitatua ili kuimarisha umaarufu wa ODM mashinani.
Alihitimisha kwa kusema kwamba chama kiko katika hatua za mwisho kuandaa mpango wa kuimarisha ODM baada ya kipindi cha maombolezo, huku akisisitiza umoja na ushirikiano kama nguzo kuu za mustakabali wa chama hicho.
Dkt Oburu alikariri kuwa hamna mipango ya kuwafurusha viongozi kama vile Sifuna na Babu Owino “kwa sababu hawajafanya kosa lolote kwa kuwa na misimamo mikali”.
“Sifuna hawezi kutimuliwa kwa sababu hamna kosa alilofanya. Sifuna ako sawa na tumeongea naye kwa sababu nyakati fulani damu yake huwa moto kwa sababu yeye ni kijana. Hata Babu Owino na wengine hawaendi popote,tunawahitaji kukipa chama chetu nguvu kuelekea uchaguzi mkuu ujao” Dkt Oginga.
Seneta huyo wa Siaya alisisitiza kuwa ajenda ya kuu wakati huu ni kupalilia umoja katika ODM baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga.
Ili kufanikisha ajenda hiyo, Dkt Oginga akaeleza, chama kinahitaji mchango wa vijana ambao kulingana naye ni viongozi wa sasa wale sio kesho.