Habari Mseto

Sonko asamehe Gen Z aliyetumia jina lake kufungua akaunti ya Facebook

Na RICHARD MUNGUTI August 16th, 2024 1 min read

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi Mike Sonko amemsamehe mwanafunzi ambaye alifungua akaunti ya Facebook kwa kutumia jina lake bila idhini yake.

Akiondoa kesi dhidi ya Tyson Kibet mwenye umri wa miaka 23, Bw Sonko alimweleza hakimu kwamba aliamua kwa hiari kumsamehe mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu bewa la Kabete.

“Niliombwa na wazazi wake ambao ni maskini na hawawezi kupata dhamana ya Sh1 milioni aliyopatiwa mtoto wao nimsamehe na kuondoa kesi,” aliambia hakimu.

Gavana wa zamani Mike Sonko akishauriana na kijana Tyson Kibet kortini. Picha|Richard Munguti

Bw Kibet amekuwa kizuizini kwa muda wa miezi mitatu baada ya kukanusha mashtaka ya kuchapisha picha zisizopendeza katika akaunti hiyo.

Bw Sonko aliambia mahakama alipokea malalamishi mengi kutoka kwa umma kuhusu maudhui ya ponografia yaliyochapishwa katika akaunti inayodaiwa kuhusishwa naye.

Alipiga ripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi na mwanafunzi huyo alikamatwa Mei 25, mwaka huu na kufikishwa mahakamani.

Mashtaka yalieleza kuwa kwa makusufi, alifungua akaunti ya Facebook kwa jina la Mike Sonko bila idhini yake, kosa ambalo anadaiwa alitenda Novemba 25, mwaka jana.

Akiondoa kesi hiyo, gavana Sonko alimtaka hakimu kusitisha kesi hiyo na kumwachilia Kibet bila masharti.