• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Cherono aibuka mfalme mpya wa Valencia Marathon

Cherono aibuka mfalme mpya wa Valencia Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Mkenya Lawrence Cherono ndiye bingwa mpya wa mbio za Valencia Marathon mwaka 2021 zilizoshuhudia ushindani mkali Jumapili.

Bingwa huyo wa Chicago na Boston Marathon, ambaye alikamata nafasi ya pili kwenye Valencia Marathon mwaka 2020, alinyakua taji kwa kukamilisha makala ya 41 kwa saa 2:05:12 mjini Valencia, Uhispania. Cherono amefuatiwa kwa karibu na Muethiopia Chalu Deso (2:05:16) na Wakenya Philemon Kacheran (2:05:19) pamoja na bingwa wa New York Marathon Geoffrey Kamworor (2:05:23).

Abebe Negewo (2:05:27), Goitom Kifle (2:05:28), Kinde Atanaw (2:05:54) na Mtanzania Gabriel Geay (2:06:10) wameridhika na nafasi ya tano hadi nane mtawalia kwenye kitengo cha wanaume kilichovutia wakimbiaji 155 wakiwemo wawekaji kasi 12.

Kabla ya mbio hizo zilizovutia washiriki 16, 000 kwa jumla, ambazo kinadada bado wanakimbia, washiriki wa kitengo cha wanaume akiwemo mshikilizi wa zamani wa rekodi ya mbio za kilomita 21 duniani Kamworor, waliaminika wana uwezo wa kuvizia rekodi ya dunia ya Eliud Kipchoge (2:01:39).

Hata hivyo, hawakufanikiwa kufanya hivyo. Pia, rekodi ya Valencia Marathon ya wanaume ya 2:03:00 iliyowekwa na Evans Chebet mwaka 2020 bado ingali imara.

You can share this post!

Rais atoa ahadi ya kuwainua walemavu

HUKU USWAHILINI: Biashara kwetu zina raha zake

T L