• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Makanisa 20 yaandaa maombi ‘kutakasa’ eneo la Turkwel linaloshuhudia mauaji kila mara

Makanisa 20 yaandaa maombi ‘kutakasa’ eneo la Turkwel linaloshuhudia mauaji kila mara

NA OSCAR KAKAI

ZAIDI ya makanisa 20 katika mpaka wa Pokot Magharibi na Turkana yameanzisha mchakato wa maombi maalum kutakasa eneo la Turkwel, ambalo hushuhudia mauaji mara kwa mara kutokana na kudorora kwa hali ya usalama.

Baadhi ya wakazi kutoka jamii zote mbili; Pokot na Turkana, wamekuwa wakizozana, mifugo kuibwa na maafa kuripotiwa.

Viongozi wa kidini, kwa ushirikiano na wa kisiasa na wakazi, walikongamana kwa maelfu wikendi kuombea eneo hilo.

Mizozo huchacha eneo la Turkwel Gorge.

Katika hafla hiyo, waliungama mgogoro wa mara kwa mara umesababisha eneo hilo kusalia nyuma kimaendeleo hivyo basi haja ipo kuunganisha jamii hasimu.

Wahubiri walihimiza jamii hizo za wafugaji kuishi kwa amani, na kuzika katika kaburi la sahau vita vya kikabila.

Wale wa kisiasa wakiongozwa na aliyekuwa Gavana wa Pokot Magharibi, John Lonyangapuo, walielezea kukerwa kwao na mivutano ya mara kwa mara.

Prof Lonyangapuo aidha aliwataka magavana wa Pokot Magharibi na Turkana, kushirikiana ili kuzima mizozo ibuka.

“Miaka mitano iliyopita tulikuwa tukihubiri amani na wenzetu kama vile Joseph Nanok, James Lomenen, Peter Lochakapong na Samuel Moroto, haswa maeneo yanayozuka ghasia. Mimi na Nanok tuliungana kukomesha vita,” alisema.

Bw Nanok alihudumu mihula miwili kama Gavana wa Turkana, 2013 – 2022.

Maombi hayo yalifanyika wiki moja baada ya mashambulizi yaliyosababisha maafa, mifugo kuibwa, wakazi kuhama makwao na mali kuharibiwa.

Septemba 2023, Shule ya Upili ya Turkwel Gorge imefungwa kwa muda kufuatia ghasia.

Ilifunguliwa mwezi jana, Oktoba 2023.

Akihimiza magavana sasa kaunti hizo mbili kuja pamoja, Prof Lonyangapuo alisisitiza umuhimu wa viongozi wote kuja pamoja ili kudumisha usalama.

“Hivi karibuni tutaunganisha magavana wa Pokot Magharibi na Turkana, na tunaomba Rais William Ruto ashiriki mkutano huo,” Gavana huyo wa zamani Pokot Magharibi akaahidi.

Bw Simon Kachapin ndiye Gavana wa Pokot Magharibi, naye Jeremiah Lomorukai Turkana.

Askofu wa kanisa la Agape, Bw Peter Siwa ambaye alikiri awali alikuwa mwizi wa mifugo kisha akabadilika, aliwataka viongozi wa kisiasa kaunti hizo mbili kuja pamoja na kuunganisha wakazi.

Alisema kwamba suala la mpaka ndio chanzo kikuu cha mizozo Turkwel, huku akiwataka viongozi kukomesha uchochezi.

“Tunaomba watu watangane na kuishi kwa Amani. Mungu anathamini Amani,” Askofu Siwa akasema.

Wakazi waliozungumza na vyombo vya habari, walisema kuwa visa vya ujangili na wizi wa mifugo vilichipuka upya 2022, baada ya miaka mitano ya utulivu.

“Amani ilikuwa imeshamiri, ila sasa tunaishi roho mikononi. Tunaomba usaidizi kutoka kwa serikali ili utulivu urejee maeneo ya Ombolion, Kainuk na Lochakula kuhubiri amani,” akasema mkazi Regina Lokorinya.

Alihuzunika wakazi wengi kupoteza watoto na familia kufuatia vita vya kijamii.

Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki ameapa kukabiliana vikali na majangili wa wizi wa mifugo Bonde la Ufa, huku vikosi vya pamoja vya usalama vikitumwa kudumisha amani.

Licha ya mikakati hiyo ya serikali, utovu wa nidhani unazidi kuripotiwa.

  • Tags

You can share this post!

Nashindwa kumsaidia mwanamume mpenzi wangu kifedha kwa...

Davis Chirchir: Huenda lita moja ya petroli ikagonga Sh300

T L