• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Mike Sonko wa mikogo na sarakasi

Mike Sonko wa mikogo na sarakasi

Na COLLINS OMULO

MAISHA ya Gavana wa Nairobi aliyetimuliwa, Mike Sonko yamejaa sarakasi hasa katika ulingo wa siasa.

Kuanzia kusemekana kupata hela kiasi cha Sh5 milioni akiwa katika Kidato cha Nne mnamo 1994, kukosana na vyombo vya sheria mwaka wa 1995 hadi akatoroka gerezani 1998 ili kuhudhuria mazishi ya mamake kabla ya kukamatwa tena, maisha yake yamekuwa sinema.

Aliposamehewa na mahakama, Bw Sonko alipanua biashara yake ya matatu aliyokuwa ameanzisha baada ya kuacha masomo ya chuo na kuhamia Nairobi kutoka Mombasa alikozaliwa.

Aliendesha biashara za vilabu vya usiku, vinyozi, maduka ya nguo, kuuza simu, ujenzi wa nyumba na pia uchukuzi wa watalii. Baadaye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha matatu za eneo la Eastlands jijini Nairobi.

Baba huyo wa watoto watatu alijikurubisha na vijana kwa kuwatetea walipokamatwa na polisi. Umaarufu wake ukapanda mnamo 2007 aliposhinda kesi kortini dhidi ya Baraza la Jiji la Nairobi wakati huo. Baraza hilo lilikuwa limetaka kuondoa matatu katikati mwa mji.

Alitumia umaarufu huo miaka mitatu baadaye mwaka wa 2010, akiwa na miaka 35 kujitosa kwenye siasa kwenye uchaguzi mdogo eneobunge la Makadara.

Kupitia chama cha Narc-Kenya na bila kujulikana kwenye ulingo wa siasa, aliwabwaga vigogo waliojumuisha wabunge wa zamani Reuben Ndolo (Orange Democratic Movement) na Dick Wathika wa PNU.

Miaka mitatu baadaye alimshinda aliyekuwa mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru na kushinda useneta wa Nairobi.

Mwaka 2017 aliwania ugavana wa Nairobi na kumshinda Dkt Evans Kidero.

Kama alivyokuwa mtu wa visanga kabla ya kuingia siasa, akiwa seneta aliwahi kupiga ukuta kwa ngumi na mateke na alikuwa daima akivaa shanga na vito vya dhahabu, jambo lililomfanya kubadili majina na kujisajili rasmi kuwa “Sonko”, jina la mtaani la mtu mwenye mali.

Kuna wakati alimpigia simu Rais Uhuru Kenyatta na kumweka kwenye spika, huku akishangiliwa na wakazi waliokuwa wavunjiwe makazi yao.

Akiwa gavana, alienda kujifurahisha ng’ambo na kurekodi video iliyoleta msemo maarufu wa ‘Party after party’ kati ya vituko vingine vingi.

Sifa yake nyingine ni kutumia matamshi ambayo inadaiwa ni ya kudunisha yeyote aliyethubutu kumpinga ama kumkosoa. Alikuwa pia na ulinzi na magari wa aina yake.

Wakati maradhi ya Covid-19 yalizuka, Bw Sonko aligonga vichwa vya habari kimataifa alipowapatia wakazi wa mitaa ya mabanda pombe aina ya Hennesey akidai ilikuwa na uwezo wa kukabili makali ya ugonjwa huo.

  • Tags

You can share this post!

Wawili wanusurika kifo Thika Road baada ya gari walimokuwa...

Sonko aliiga Trump kuongoza