• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Thugge kuondoa sheria inayozuia Wakenya kuweka na kutoa kwa benki Sh1 milioni na zaidi

Thugge kuondoa sheria inayozuia Wakenya kuweka na kutoa kwa benki Sh1 milioni na zaidi

NA CHARLES WASONGA

WAKENYA wataweza kuweka na kutoa zaidi ya Sh1 milioni kutoka mashirika ya kifedha ikiwa wabunge wataidhinisha uteuzi wa Kamau Thugge kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Jumanne, Dkt Thugge amewaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango kwamba atapendekeza sheria kuhusu suala hilo ifanyiwe mabadiliko.

“Nafahamu kwamba vikwazo hivi viliwekwa na sehemu 33 ya Sheria ya Benki ili kuzuia ulanguzi wa fedha na uhalifu wa kifedha kwa ujumla. Lakini endapo Kamati hii itaidhinisha uteuzi wangu kama Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, nitawasilisha pendekezo la sheria hii kufanyiwa marekebisho japo kwa kuweka viunzi vya kuzuia wahalifu kupata mwanya wa kushiriki ulanguzi wa fedha,” akasema.

Dkt Thugge alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Chesumei Paul Biegon ambaye alitaka kujua hatua ambayo atakuwa kuhakikisha kuwa watu kutoka jamii ya wafugaji wanaweza kuweka katika benki zaidi ya Sh 1 milioni baada ya kuuza mifugo wao.

Kulingana na Sheria hiyo iliyoanza kutekelezwa mnamo 2018, mtu yeyote anayepania kuweka au kutoa Sh1 milioni na zaidi kutoka kwa mashirika ya kifedha nchini sharti aelezee, kwa maandishi, chanzo cha pesa hizo au jinsi anavyopania kuzitumia.

Dkt Thugge alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kupigwa msasa kuhusu ufaafu wake kushikilia wadhifa wa Gavana wa CBK.

Hii ni baada yake kuteuliwa na Rais William Ruto majuma mawili miongoni mwa watu kadha waliomba kazi hiyo.

Ikiwa wabunge wataidhinisha uteuzi wa Dkt Thugge, atamrithi Dkt Patrick Njoroge ambaye muhula wake wa miaka sita unakamilika mnamo Juni 20, 2023.

Dkt Thugge ambaye ni mshauri wa Rais kuhusu masuala ya uchumi, pia alitumia fursa hiyo kujitetea dhidi ya kuhusishwa kwake na sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

“Narudia hapa kwamba niliondolewa lawama na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kwa sababu suala hilo halikuhusu Wizara ya Fedha ambako nilihudumu kama Katibu. Lakini sasa nimegeuzwa kuwa shahidi wa serikali na nitashirikiana na mahakama nikihitajika,” akasema.

Kuhusu utajiri wake, Dkt Thugge amesema kuwa anamiliki mali ya thamani ya Sh450 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Atwoli atengwa vyama vikipinga mswada wa Ruto

Ziara za Rais ugenini raia wakikaza mshipi

T L